1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Uganda inatumia suala la COVID-19 kukandamiza upinzani

20 Novemba 2020

Mwanasiasa wa Uganda, Robert Kyagulanyi ameachiwa huru kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa kukiuka masharti ya kudhibiti COVID-19. Human Rights Watch imesema kukamatwa kwake ni ishara ya kuongezeka kwa ukandamizaji 

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Picha: REUTERS

Mnamo Novemba 18, vikosi vya usalama nchini Uganda vilimkamata Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, katika wilaya ya Luuka mashariki mwa nchi hiyo, alipokuwa akijiandaa kwa kampeni iliyopangwa eneo hilo.

Msemaji wa polisi Fred Enanga alisema kupitia taarifa kwamba Kyagulanyi ambaye ni mgombea urais wa chama cha National Unity Platform, Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) alitiwa mbaroni kwa madai ya kukiuka masharti ya kudhibiti ugonjwa wa COVID-19, kwa kuwahimiza wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni zake.

Maandamano ya vurugu yalizuka katika mji wa Kampala na mingineyo kufuatia kukamatwa kwake. Maafisa wa usalama walitumia mabomu ya kutoa machozi pamoja na risasi za moto dhidi yao. Polisi imesema idadi ya watu waliuawa imefikia 37.

Oryem Nyeko ambaye ni mtafiti wa masuala ya Afrika katika shirika la Human Rights Watch amesema kuongezeka kwa machafuko mapema hivi kwenye kipindi cha kampeni, hakuleti taswira nzuri kuhusu wiki zijazo kabla ya uchaguzi.

Mauaji yachunguzwe, HRW

Nyeko amesema maafisa wanaweza kuepusha ghasia zaidi kutokea kwa kuacha kuwanyanyasa waandishi wa habari, wanasiasa wa upinzani pamoja na wafuasi wao, na waache kuvuruga kampeni zao kwa fujo.

Shirika hilo limetoa wito kutaka mauaji ya watu yachunguzwe, hatua ya wapinzani kukamatwa kiholela ikomeshwe na watu waruhusiwe kukusanyika kwa amani.

Nyeko amesema mara kwa mara, maafisa wametumia vikwazo vya kudhibiti COVID-19 kama kisingizio cha kuwakandamiza wapinzani badala ya kulinda kidemokrasia kufanikisha uchaguzi wa haki na huru.

Mfuasi wa Bobi Wine akiwa amebebwa mzobemzobePicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Polisi wawajibishwe, HRW
Ameongeza kuwa badala yake, serikali ya Uganda inapaswa kuhakikisha maafisa wa usalama wanaheshimu utawala wa sheria, wanawajibishwa kutokana na maovu yao na wasiegemee upande wowote katika utendakazi wao.

Siku sawa na aliyokamatwa Kyagulanyi, polisi walimkamata mgombea mwengine wa urais wa upinzani wa chama cha Forum for Democratic Change-FDC, Patrick Oboi Amurait, eneo la Gulu kaskazini mwa Uganda. Lakini akaachiliwa huru baadaye. Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa mgombea huyo wa FDC kukamatwa katika kipindi cha siku mbili kwa madai ya kupanga maandamano ambayo hayakuruhusiwa.

Katika picha za video ambazo zinasambaa katika mitandao ya kijamii, watu waliovalia kiraia huku wakiwa na bunduki huku wakifyatua angani, wanaonekana wakishirikiana na polisi kuwatawanya waandamanaji. Shirika la Human Rights Watch halijathibitisha video hiyo.

Mshindani mkuu wa Rais Museveni Bobi Wine


Ukandamizaji dhidi ya upinzani Uganda-HRW

Katika wiki mbili zilizopita, maafisa wa serikali Uganda wametumia masharti ya kudhibiti COVID-19 kama kijisababu kukiuka haki na kuwakandamiza wapinzani pamoja na vyombo vya habari.

Wamewakamata wanasiasa wa upinzani, waandishi wa habari huku wakivunja kampeni za upinzani wakitumia mabomu ya kutoa machozi kwa madai ya kukiuka masharti kuhusu COVID-19. Lakini licha ya chama tawala National Resistance Movement (NRM) chake Rais Yoweri Museveni pia kuwa na umati mkubwa kwenye kampeni, vikosi vya usalama vimeruhusu kampeni hizo kuendelea bila ya kuvurugwa.

Mnamo Novemba 3, polisi walivunja dirisha la gari la Kyagulanyi wakijaribu kumkamata katika chuo kikuu cha Kyambogo mjini Kampala, punde tu baada ya tume ya uchaguzi kuthibitisha uteuzi wake kama mgombea urais.
Kyagulanyi aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi walimnyunyizia dawa yenye kemikali machoni wakati alipokuwa akikamatwa.

Mapema mwaka huu, wakati maafisa wa polisi walipokuwa wakitekeleza masharti ya kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona, waliwapiga raia risasi, kuwapiga na kuwakamata mamia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW