HRW: Uvunjifu wa haki za binaadamu washamiri Afrika
18 Januari 2018Ripoti hiyo iliyoangazia uvunjifu wa haki za binaadamu katika mataifa ya Afrika Mashariki imesema nchini Kenya mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kutetea haki za binaadamu yalikusanya takwimu zinazoonyesha visa kadhaa vya ukiukwaji wa haki na ukatili unaodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama katika operesheni za kijeshi na za kudumisha sheria kati ya mwaka 2016 na 2017 nchini Kote, hali hii ikikithiri hasa katika kipindi cha uchaguzi.
Shirika la Human Rights watch lilibaini kuwa mauaji yaliyofanywa na polisi katika mitaa ya mabanda kama vile Mathare Kayole Huruma Dandora, Huruma Eastleigh kibera na Kariobangi, hayakuchunguzwa hadi wa leo.
Aidha katika kipindi cha kabla na baada ya uchaguzi shirika hilo limesema polisi na vikosi vengine vya usalama viliztumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji hasaa katika ngome za upinzani.
Maandamano hayo yalizuka baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kudai kura za uchaguzi wa Agosti mwaka 2017 zilikuwa zimeibwa.
Uhuru wa kujieleza na vitisho dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni mambo yaliyotajwa kutokea nchini Kenya katika ripoti hiyo ya Human Rights Watch
Katika nchi jirani ya Tanzania shirika hilo limesema baada ya rais John Pombe magufuli kuingia madarakani Oktoba mwaka 2015 alidhamiria kuondoa tatizo la rushwa serikalini na kuongeza uwajibikaji kwa manufaa ya wananchi wa kawaida lakini badala yake amezuwiya uhuru wa msingi kupitia sheria na matamko kandamizi.
Waandishi habari, wakosoaji wanasiasa watetezi wa haki za binaadamu na wanaharakati wa asasi za kiraia wamekumbana na aina mbali mbali za vitisho na kuwekwa vizuizini bila sababu za msingi kunakofanywa na mamlaka za serikali. Uhuru wa vyombo vya habari pia haukunusurika hali iliyoshuhudiwa vyombo vya habari kadhaa vikifungiwa kufuatia ripoti zinazoikosoa serikali.
Tukiiangazia serikali ya Uganda ya Rais Yoweri Museveni iliyo madarakani tangu mwaka 1986, ripoti ya Human Rights Watch inasema inaendelea kukiuka haki za binaadamu uhuru wa kujieleza na haki za bunge.
Maandamano yaliyofanyika kupinga mabadiliko katika katiba ya nchi hiyo ya kuondoa ukomo wa umri wa rais hali inayomuezesha sasa rais Museveni kuendelea kuwania kiti hicho cha urais mwaka 2021, yalijibiwa kwa nguvu kali na maafisa wa polisi. Maafisa wa polisi wanaendelea kutumia nguvu kupita kiasi huku wakilindwa.
Kwa mfano hakukuwepo na uchunguzi wa aina yoyote kwa tukio la Novemba mwaka 2016 wakati jeshi na polisi walipofanya mashambulizi katika eneo la kasese yaliyowauwa watu zaidi ya 100 wakiwemo watoto lilisema shirika hilo la Human Rights Watch.
Nchini Rwanda serikali ya rais Paul Kagame inasemekana kuweka mipaka kwa mashirika yasiyo yakiserikali, wapinzani wa kisiasa kwa kufuatilia namna wanavyofanya kazi na kutokuwa na sauti ya moja kwa moja ya kuikosoa sera za serikali na namna inayowatumikia wananchi wake.
Shirka la Human Rights watch limesema taifa hilo limekuwa likiwauwa watu waliyofanya makosa madogo madogo na wale wanaoikosoa serikali wanajikuta kororoni wanakopokea mateso makubwa, huku likisema uvunjifu wa haki za binaadamu na hali ya ati ati ya kisiasa nchini Burundi iliyoanza mwaka 2015 wakati rais Pierre Nkurunzinza alipotangaza kuwania muhula mwengine madarakani kunazidisha uwepo wa visa vya ubakaji, mauaji na madhila mengine yanayofanywa na vikosi vya usalama na jeshi.
Hali ambayo inazidi kuongeza wimbi kubwa la wakimbizi wanaotorokea nchi jirani wakihofia usalama wao nchini Burundi.
Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mambo ni yale yale yaliyoripotiwa na shirika hilo la kutetea haki za binaadamu kwamba, mgogoro wa kiasiasa na serikali kukandamiza upinzani umeendelea kushuhudiwa mwaka 2017 wakati rais Joseph Kabila akiendelea kubakia madarakani.
Mwandishi Amina Abubakar/Human Rights Watch
Mhariri: Daniel Gakuba