1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Waasi wa CODECO walifanya mauaji ya kikatili Ituri, DRC

27 Julai 2023

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema wiki hii kuwa waasi wa CODECO waliwauwa Juni 12, 2023 takriban raia 46 katika kambi ya wakimbizi mkoani Ituri mashariki mwa DRC.

DR Kongo Rethy | militante Milizgruppe URDPC/CODECO
Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kundi linalojiita Ushirika wa Maendeleo ya Kongo (CODECO), lenye wanamgambo wengi kutoka kabila la Lendu, wamekuwa wakishambulia mara kwa mara kambi za watu waliokimbia makazi yao huko Ituri.

Wanamgambo hao walishambulia nyakati za usiku kambi ya Lala , ambayo ilikuwa inawahifadhi wakimbizi wengi wa ndani kutoka kabila la Hema. Wapiganaji hao waliendesha mauaji hayo kwa kuwapiga risasi, kuwakata mapanga, au kuwachoma moto watoto wapatao 23, wanawake 13 na wanaume 10, na kuwajeruhi watu wengine 8. Wanajeshi wa Kongo pamoja na kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa waliokuwa katika mji ulio karibu wa Bule hawakuingilia kati.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW)Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Thomas Fessy, mtafiti mkuu anayehusika na Kongo katika shirika hilo la Human Rights Watch amesema imekuwa jambo la kawaida kwa kundi la CODECO kuwashambulia raia katika kambi wanakotafuta kimbilio kutokana na ghasia na kwamba kambi hizi zinapaswa kuwa maeneo salama badala ya maeneo ya mauaji. 

Fessy ameendelea kuwa ni muhimu kwa Jeshi la Kongo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lao la ulinzi ili kuhakikisha kuwa watu waliokimbia makazi yao wako salama.

Soma pia: Zaidi ya raia 45 wauawa baada ya kushambuliwa na wanamgambo, Ituri

Matukio ya sasa ya ghasia na kulipiza kisasi yanayojirudia huko Ituri, na ambayo yalianza Desemba mwaka 2017, yanatokana na masuala ya muda mrefu ambayo hayajashughulikiwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati makumi kwa maelfu ya raia walikufa katika mauaji ya miaka 1999 hadi 2007.

Soma pia: Zaidi ya raia 150 wauawa Kongo katika wiki mbili: UN

Migogoro iliyorithiwa kutokana na ukosefu wa usawa wakati wa enzi za ukoloni kama vile haki za umiliki wa ardhi, mahusiano ya kikabila, uingiliaji wa masuala ya kikanda na udhibiti wa maliasili kati ya jamii, hasa zile za Wahema na Lendu, lilikuwa na bado linaendelea kuwa kiini cha matatizo hayo.

Jeshi la Kongo na MONUSCO walaumiwa

Wakati mauaji hayo ya kinyama yakiendelea, wakimbizi na wakaazi wa kijiji jirani cha Lodinga, walipiga simu na kutoa tahadhari kwa wanajeshi wa Kongo na vikosi vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo (MONUSCO), lakini hawakupata msaada wowote.

Soma pia: Watu 41 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya wakimbizi Mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Picha: Alain Uaykani/Xinhua/IMAGO

Mwanamume wa miaka 32 kutoka kabila la Hema amesema kulikuwa na moto ambao moshi wake ungeweza kuonekana kwa mbali na kulikuwa na milio ya risasi ambayo wanajeshi hao wangeweza pia kuisikia, lakini hawakuja kuwaokoa. Manusura huyo amesema kuwa hajui kitakachowatokea ikiwa serikali itawaacha bila ulinzi wowote kambini hapo.

Human Rights Watch ilizungumza kwa njia ya simu na manusura tisa pamoja na mashahidi wengine ambao walisema waliamshwa na milio ya risasi wakati wapiganaji wakiishambulia kambi hiyo.

Soma pia: Vikosi vya UN vimefanikiwa kuzuia jaribio la shambulizi DRC

Wanajeshi wa Kongo walikuwa katika kituo chenye umbali wa kilomita 1.5 lakini waliwasili kambini hapo baada ya jua kuchomoza na wanamgambo kuondoka, na walikuja kusaidia kukusanya maiti na kuhakiki waliojeruhiwa.

Kifaru cha Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO)Picha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Nao askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, waliokuwepo umbali wa kilomita sita katika kambi moja huko Bule, hawakuweza pia kuingilia kati.

Afisa mkuu wa Ujumbe huo, Meja Imran Tareq, ameiambia Human Rights Watch kwamba walishindwa kufika eneo la tukio kutokana na kifaru kimoja kuharibika na hivyo kushindwa kutimiza sharti la kuwa na msafara wa magari mawili kama inavyoagiza kanuni wakati wa operesheni kama hizo.

Hata hivyo, idara ya Operesheni za kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa  imeiambia Human Rights Watch kwamba MONUSCO inafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo, na iwapo uchunguzi utabaini kuwa wanajeshi hao hawakutimiza wajibu wao na bila sababu zozote za msingi, basi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Chanzo: (HRW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW