1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Wasichana walikuwa wahanga wa unyanyasaji kingono Kasai

Sylvia Mwehozi
22 Mei 2019

Ripoti ya shirika la Muungano wa ulinzi wa elimu dhidi ya Mashambulizi kwa kushirikiana na Human Rights Watch inasema wasichana walikumbwa na unyanyasaji wa kingono wakati wanamgambo walipozishambulia shule huko Kasai.

Kongo Kananga - Hungersnot: Mütter mit Kindern warten auf Nahrungsmitteln
Picha: picture-alliance/dpa/K. Bartlett

Vurugu hizo ziliwaathiri watoto wote lakini wasichana ndio walikuwa wahanga wakubwa wa unyanyasaji ikiwemo kubakwa na kuolewa na wanamgambo. Ripoti hiyo yenye kurasa 76 imezingatia mahojiano 55 yaliyofanywa na wanafunzi wa kike, walimu na wakuu wa shule ambazo zilishambuliwa katika mkoa huo. Wanafunzi na walimu wa kike walibakwa na kulazimishwa kuolewa na wanamgambo.

Baadhi yao walilazimishwa pia kujiunga na makundi ya wapiganaji wakitumika kama ngao katika uwanja wa mapambano bila ya kujihami, kwasababu iliaminika kuwa wasichana hao walikuwa na ulinzi wa nguvu za kimazingara kuvilinda vikosi hivyo vya wanamgambo.

Watoto wengi wanaaminika kuuawa na vikosi vya usalama vya Congo ikiwemo wasichana wengi ambao walitumiwa kama ngao. Jeshi la Congo FARDC pia lilishambulia shule takribani 38 katikati mwa mkoa wa Kasai na kufanya uhalifu wakati walipolilenga kundi la wanamgambo la Kamuina Nsapu. Uhalifu huo ni pamoja na kuwalenga raia, utekaji, ubakaji na unyanyasaji mwingine.

Afisa wa Shirika la kimataifa la Uhamiaji IOM akikusanya data mwamiaji wa congo Picha: Reuters/G. Paravicini

Maafisa kadhaa wa jeshi hilo wanashukiwa kufanya uhalifu ikiwemo mauaji na unyanyasaji wa kingono mashariki mwa Congo kati ya mwaka 1998-2013. Ripoti inaeleza kuwa pande zote, yani jeshi la Congo na lile la Kamuina Nsapu, walitumia shule kwa ajili ya shughuli za kijeshi. mkurugenzi wa Muungano wa ulinzi wa kimataifa wa elimu Diya Nijihowne aliieleza DW kuwa.

"Mamia ya shule zilivamiwa kwasababu ziliwakilisha majengo ya kiraia kwahiyo ilikuwa rahisi kulengwa na wanamgambo. Wasichana walibakwa, kutekwa na kusajiliwa na makundi ya wanamgambo ambao waliamini kuwa wasichana wana nguvu za kichawi na kuwatumia kama ngao dhidi ya wanajeshi waliokuwa na silaha, wao walijikinga tu kwa mifagio na vyombo vya jikoni na matokeo yake ni kwamba wengi waliuawa ", alisema Nijihowne. Soma zaidi..

Walimu na wanafunzi hawakuwa na taarifa za kutosha kuhusu mashambulizi na mara nyingi mashambulizi yalikuwa ya kushutukiza. Wakuu wa shule na walimu wanasema hawakupokea taarifa yoyote juu ya kitisho cha mashambulizi kutoka kwa mamlaka za mkoa na serikali au hata vikosi vya usalama katika mkoa huo. Kwa maana hiyo hawakujua jinsi ya kukabiliana na kujilinda dhidi ya mashambulizi, wala mafunzo ya kiusalama au taarifa juu ya hatari ambazo zingejitokeza.

Wahamiaji wa Congo wakivuka mpaka kuingia Angola Picha: Reuters/G. Paravicini

Ingawa wavulana na wasichana wote elimu yao ilitatizwa, wasichana waliathirika zaidi kwasababu ya kushindwa kurejea shuleni. Mzozo huo ulisababisha hali ya kiuchumi katika mkoa huo kuwa mbaya sana. Wazazi waliposhindwa kuwalipia karo watoto wote ilibidi wachague kuwalipia ada watoto wa kiume pekee kuendelea na masomo.

Mnamo Mei 2016, serikali ya Congo ilichukua hatua muhimu za ulinzi wa elimu kwa kuidhinisha mkataba wa kimataifa wa usalama wa shule, ambao una wajibu wa kuwalinda wanafunzi, walimu na vyuo dhidi ya mashambulizi ya vikosi vilivyo na silaha sambamba na makundi ya wanamgambo. Diya anasema licha ya kuridhia mkataba huo ni lazima uchunguzi ufanyike na wahusika wawajibishwe.

"Wafanye uchunguzi na kuwafungulia mashitaka wahusika wa unyanyasi kingono katika jimbo la Kasai na wanahitaji kuongeza mafunzo ya kiusalama. na yeyote ambaye ameshitakiwa kwa uhalifu huo asiruhusiwe kuwa sehemu ya vikosi vya usalama kote nchini."

Tangu mwezi Mei 2017, nchi 87 duniani kote zimetia saini mkataba huo wa kimataifa wa Usalama wa shule. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW