1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Watoto Kaskazini mwa Nigeria wamekoseshwa elimu

Admin.WagnerD12 Aprili 2016

Ripoti mpya ya Human Rights Watch inasema mashambulizi ya Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa Nigeria dhidi ya shule, wanafunzi na walimu yamewaacha watoto zaidi ya milioni moja bila fursa ya elimu.

Magofu ya mojawapo ya majengo ya shule zilizoharibiwa na Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa Nigeria
Magofu ya mojawapo ya majengo ya shule zilizoharibiwa na Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa NigeriaPicha: AMINU ABUBAKAR/AFP/Getty Images

Ikiwa na kichwa cha habari kisemacho, ''Wanazichoma moto shule, na kuishambulia elimu Kaskazini Mashariki mwa Nigeria'', ripoti hiyo ya shirika la Human Rights Watch yenye kurasa 86 inaeleza kwa kinaganaga ukatili ambao Boko Haram imekuwa ikiwafanyia wanafunzi, walimu pamoja na shule zao, katika majimbo ya Kano, Borno na Yobe tangu mwaka 2009.

Inaelezwa katika ripoti kwamba kuanzia mwaka 2009 hadi 2015, Boko Haram iliziharibu shule 910 na kuzilazimisha nyingine zaidi ya 1500 kufunga milango. Katika kipindi hicho hicho, inaeleza ripoti hiyo, walimu 611 wameuawa, na wengine 19,000 wamelazimika kukimbia.

Mmoja wa maafisa waliofanya utafiti na kuandika ripoti, Mausi Segun ameiambia DW, kwamba hata walimu wachache waliobaki wamepata mshituko na wanaishi kwa wasiwasi.

''Wengi wao wanaishi katika makambi ya wakimbizi wa ndani. Baadhi yao wanafanya kazi za serikali na wanapata mshahara mdogo, ambao wanasema haufiki kwa wakati, huku wakiwa na familia na marafiki wanaopaswa kuwahudumia. Wengi wao wamepata mshituko wa kudumu maisha yao yote, kwa sababu wameshuhudia wenzao na watu wa familia zao wakiuawa.'' Amesema Segun.

Jeshi la serikali lawamani

Kundi hilo lenye itikadi kali za kiislamu vile vile limewateka nyara raia zaidi ya 2000, wengi wao wakiwa wanawake na wasichana, wakiwemo wale waliochukuliwa katika makundi makubwa ya wanafunzi.

Wasichana 219 wa shule ya Chibok waliotekwa na Boko Haram miaka 2 iliyopita bado hawajapatikanaPicha: Reuters

Mtafiti Mausi Segun amelilaumu jeshi la Nigeria kuchangia katika matatizo hayo, kwa kuweka kambi zao katika shule. Segun anasema ingawa hatua hiyo ilichukuliwa kwa malengo ya kuzilinda shule hizo, kuwepo kwa wanajeshi kulizifanya kuwa shabaha ya waasi wa Boko Haram. Kwa upande mwingine, amesema Mausi Segun, wanajeshi wa Nigeria pia walizishambulia shule ambako wapiganaji wa Boko Haram waliweka kambi zao.

Miaka miwili baadaye, wasichana wa Chibok bado hawajapatikana

Shambulizi la Boko Haram kwenye shule ya bweni ya Chibok tarehe 14 Aprili mwaka 2014, ambapo wasichana 276 wa shule hiyo walichukuliwa mateka, limekuwa nembo ya njama za kundi hilo kuikandamiza elimu. Wasichana 219 miongoni mwa hao waliotekwa nyara bado hawajapatikana, takriban miaka miwili tangu walipokamatwa.

Wanajeshi wa Nigeria wanalaumiwa kutoushughulikia ipasavyo mzozo wa Boko HaramPicha: picture-alliance/dpa/Ngala Chimtom

Human Rights Watch inasema katika ripoti yake, kwamba ukandamizaji wa Boko Haram dhidi ya kile inachokiita ''Elimu ya Kimagharibi'' ulianza kudhihirika mwaka 2012, ambapo kundi hilo lilianza kuchoma shule na kuharibu mali na majengo ya shule, likidai lilikuwa likilipa kisasi vitendo vya serikali dhidi ya shule za korani.

Ukatili wa Boko haram ulikithiri pale jeshi la Nigeria lilipoanza kuliandama kundi hilo kuanzia mwishoni mwa mwaka 2012, likaanza kuuwa walimu na maafisa katika sekta ya elimu.

Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari aliingia madarakani akiapa kuitokomeza Boko Haram, lakini tayari watu zaidi ya 1000 wameuawa na kundi hilo tangu alipoingia uongozini.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mhariri:Iddi Ssessanga

http://www.dw.com/en/hrw-generation-robbed-of-their-rights-to-education-in-nigeria/a-19179416

https://www.hrw.org/report/2016/04/11/they-set-classrooms-fire/attacks-education-northeast-nigeria

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW