HRW yabaini madhila ya wahamiaji, Libya
25 Januari 2019Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Human Rights Watch inasema sera za Umoja wa Ulaya zinachangia mzunguko wa mateso yaliyokithiri dhidi ya wahamiaji nchini Libya.
Ripoti hiyo yenye kurasa 70 iliyopewa jina la "hakuna kutoroka kuzimu", imeorodhesha tabu wanazopata wahamiaji ikiwa ni pamoja na msongamano mkubwa, huduma mbaya za vyoo, utapiamlo na kukosekana kwa huduma za afya. Human Rights Watch imebaini unyanyasaji wa kikatili unaotekelezwa na walinzi wa pwani ya Libya katika vituo vinne vya kuwahifadhi wakimbizi huko magharibi mwa Libya, ikiwa ni pamoja na kupigwa na kuchapwa viboko.
Shirika hilo lilishuhudia idadi kubwa ya watoto wakiwemo watoto wachanga wakishikiliwa katik amazingira hafifu kwenye vituo 3 kati ya vinne. Karibu asilimia 20 ya wale walioingia Ulaya kupitia bahari mwaka 2018 walikuwa ni watoto.
Mkurugezi anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya katika shirika hilo Judith Sunderland amesema "wahamiaji na waomba hifadhi wanaoshikiliwa Libya, ikiwa ni pamoja na watoto wamekwama katika jinamizi na kinachofanywa na serikali za Umoja wa Ulaya kinazidisha makali badala ya kuwatoa watu katika mazingira ya unyanyasaji".
Ripoti hiyo inazitaka mamlaka za Libya kuheshimu haki za wahamiaji na wakimbizi, na kwamba ushiriki wa Umoja wa Ulaya huko Libya uwe wa kibinadamu. Human Rights Watch ilizungumza na zaidi ya wahamiaji 100 pamoja na waomba hifadhi, wakiwemo watoto 8 ambao hawana mtu, pamoja na wakuu wa vituo hivyo na wafanyakazi. Maafisa wa ngazi ya juu katika taasisi za Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wanafahamu juu ya hali hiyo. Mwezi Novemba mwaka 2017, Kamishina wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitri Avramopoulos alisema kuwa " sote tunatambua na kufahamu mazingira mabaya wanayoshikiliwa wahamiaji Libya", akiongeza kuwa tangu mwaka 2016, Umoja wa Ulaya na hasa nchi wanachama wamemwaga mamilioni ya euro kufadhili programu za kuimarisha uwezo wa walinzi wa Pwani kukabiliana na boti zinazoondoka Libya".
Italia nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambayo, wahamaiji wengi wamewasili kutoka Libya imekuwa kinara katika kutoa vifaa na usaidizi wa kiufundi kwa walinzi wa Pwani wa Libya na kuchukua majukumu karibu yote ya kuratibu operesheni za uokoaji baharini, ili kuzuia kiwango cha watu wanaowasili kwenye pwani zake.
Mamlaka za Libya zinapaswa kukomesha ukatili huo dhidi ya wahamiaji walioko kizuizini, kuboresha hali katika vituo vya mahabusu na kuhakikisha uwajibikaji kwa serikali na watendaji wasio wa serikali wanaokiuka haki za wahamiaji na waomba hifadhi. Shirika hilo pia linaitaka Libya itie saini makubaliano na shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR ili waweze kumwandikisha kila mtu anayehitaji ulinzi wa kimataifa bila ya kujali uraia wake.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/HRW
Mhariri: Yusuf Saumu