1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yahofia wafungwa zaidi walikufa kwenye moto Burundi

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
24 Januari 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema huenda mamia zaidi ya wafungwa walikufa na pia watu zaidi walijeruhiwa katika maafa ya moto kwenye gereza la Gitega nchini Burundi.

Burundi Gefängnis Feuer Brand Gitega
Picha: ASSOCIATED PRESS/AP/picture alliance

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linaitaka serikali ya Burungi ifanye uchunguzi na itoe habari za kuaminika juu ya maafa ya moto yaliyosababisha vifo kwenye gereza la Gitega ili kuleta haki. Kwa mujibu wa taarifa mamia ya wafungwa walikufa na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Mpaka sasa serikali ya Burundi bado haijafanya uchunguzi wa haki juu ya maafa hayo ya moto ili kubainisha mazingira yaliyosababisha moto huo na jinsi ulivyoenea na wala haijatoa  taarifa kueleza jinsi walivyojaribu kuudhibiti au iwapo walijaribu kuwaokoa wafungwa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linaitaka serikali ya Burundi itoe taarifa ya uwazi na itoe orodha ya majina ya wafungwa waliokufa na watu waliojeruhiwa. Asasi hiyo inaitaka serikali ya Burundi iwafungulie mashtaka wale waliohusika na chanzo cha moto huo. Pia serikali hiyo inatakiwa itoe fidia kwa familia za wahanga na matibabu kwa waliojeruhiwa. Ndugu na jamaa pia wapewe msaada unaohitajika.

Gereza la Gitega nchini BurundiPicha: ASSOCIATED PRESS/AP/picture alliance

Mkurugenzi wa asasi ya Human Rights Watch kanda ya Afrika ya kati Lewis Mudge amesema sasa umeshapita mwezi mmoja tangu kutokea kwa mkasa huo kwenye gereza la Gitega lakini serikali ya Burundi bado haijatoa taarifa kamili kwa familia za wahusika. Amesema ukimya wa serikali juu ya wafungwa waliokufa na waliojeruhiwa unaongeza machungu kwa familia hizo.

Kwa mijubu wa taarifa moto ulizuka alfajiri tarehe 7 mwezi uliopita kwenye gereza hilo lililopo katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura. Ulianza kuenea kwenye majengo na nyumba kadhaa ambamo mamia ya wafungwa wanaweza kuwekwa.

Wafungwa watatu pamoja na mtu mwengine waliohojiwa wamesema jengo la nne la jela lenye uwezo wa kuchukua wafungwa hadi 250 ndilo lililokumbwa na maafa ya moto huo kwa kiwango kikubwa zaidi. Wamesema wafungwa waliojaribu kujiokoa walilazimika kubomoa ukuta. Baadhi ya wafungwa wamesema juhudi za uokozi hazikufanyikla haraka. Waokozi walifika kati ya saa 11 na nusu na saa 12 asubuhi baada ya moto kuzuka saa 10 alfajiri.

Kulingana na maelezo ya mfungwa mmoja aliyehojiwa kwa njia ya simu, wafungwa wengi kwenye jengo lao walinusurika lakini amesema kwenye majengo mengine wafungwa hawakuwahi kuamka na kwa hivyo wengi walikufa.  Amesema walinzi walifika saa 12 asubuhi lakini walikuwa wamechelewa na baadhi aa wafungwa walivuta moshi na kufa.

Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Giscard Kusema

Makamu wa rais wa Burundi Prosper Bazombanza aliwaambia waandishi habari kwamba waliokufa walikuwa 38 lakini hakutaja majina yao. Wizara ya mambo ya ndani ya Burundi imesema moto huo ulisababishwa na hitilafu kwenye waya za umeme.

Wiki kadhaa baadaye rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alitaja idadi ya waliokufa kuwa ni 46 pamoja na mtu mwingine aliyefia hospitalini. Hata hivyo mfungwa mmoja ameliambia shirika la haki za binadamu kuwa idadi hiyo si ya kweli. Mfungwa huyo amedai kwamba waliokufa ni kati ya watu 200 na 400.

Baadhi ya watu wamesema hawajapewa taarifa kamili juu ya ndugu zao waliokufa. Wafungwa wengi kwenye jela ya Gitega na jela zingine ni watu waliofungwa kwa sababu ya kushiriki katika harakati za amani za kisiasa.

Chanzo:  https://www.hrw.org/afrique/burundi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW