1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaishutumu Rwanda kwa mauaji ya wakosoaji nje ya nchi

10 Oktoba 2023

Shirika la Human Rights Watch (HRW) linaituhumu serikali ya Rwanda kuhusika na vifo, mashambulizi na kupotea kwa wakosoaji wake walio nje na linaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kusimamisha ukandamizaji huo.

Ruanda Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda anatuhumiwa na HRW kuwaandamana wapinzani wake walio nje ya nchi.Picha: Trinidad Express Newspaper/AFP

Ripoti iliyochapishwa siku ya Jumanne (Oktoba 10) na shirika hilo la kimataifa la haki za binaadamu inasema taifa hilo dogo limekuwa likiongozwa kimsingi na Rais Paul Kagame tangu mauaji ya maangamizi ya mwaka 1994, na kwamba sasa kiongozi huyo anataka kuendelea kutawala kupitia uchaguzi ujao hapo mwakani.

"Ili kuendelea kushikilia madaraka, chama tawala cha RPF kimekuwa kikitumia nguvu na ukandamizaji dhidi ya yeyote anayeonesha upinzani dhidi yake," Inasomeka sehemu ya ripoti hiyo,

Utafiti uliofanywa na shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani unaonesha kuwa hatua hizo za serikali ya Rwanda haziishii kwa wapinzani wa ndani tu, bali kuna matukio zaidi ya kumi ambayo yametokea nje ya nchi yakiashiria kuwa Kigali ina mkono wake.

Mabango ya watu wanaopinga kuhamishiwa wahamiaji wa Uingereza kupelekwa Rwanda.Picha: Tom Pilgrim/empics/picture alliance

Soma zaidi: Rwanda yatakiwa kuheshimu Uhuru wa Kujieleza

Ripoti hiyo ambayo imeandikwa baada ya mahojiano na zaidi ya watu 150, ikijikita kwenye kipindi cha baina ya mwaka 2017 wakati Kagame alipochaguliwa tena hadi mwaka huu, inataja visa vya watu wanaochukuliwa kuwa ni wapinzani wa Kagame nje ya nchi kuuawa, kutekwa, kupotezwa na ama kushambuliwa na pia juhudi za kuwalazimisha kurudi nyumbani wakosoaji hao. 

Rwanda yakanusha

Alipoombwa na shirika la habari la AFP kutoa kauli yake juu ya ripoti hiyo ya Human Rights Watch, msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alisema shirika hilo linaendelea "kuwasilisha taswira isiyo sahihi ya Rwanda, ambayo imo kwenye dhana zao tu." 

Ripoti hiyo ya HRW imetolewa wakati Mahakama ya Juu nchini Uingereza ikiendelea na vikao vyake vya siku tatu kusikiliza ombi la rufaa la serikali ya nchi hiyo ambayo inapinga uamuzi wa kuzuiliwa mipango yake ya kuwahamishia waomba hifadhi nchini Rwanda.

Rwanda yatuhumiwa kuwashambulia wakosoaji wake walioko nje

This browser does not support the audio element.

Soma zaidi: Mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda akamatwa Uholanzi

 "Uvunjaji huu wa wazi wa haki za binaadamu unazusha wasiwasi, hasa hasa ndani ya mataifa ya Afrika na mataifa mengine ambako serikali ya Rwanda ina ushawishi wake, ukiwemo ushawishi wa kijeshi. Kwenye baadhi ya matukio, kuna nchi zimeshirikiana na Rwanda ama angalau zimefumbia macho matendo hayo yanapotokea kwenye ardhi zao." Inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Nchini Msumbiji, ambako vikosi vya Rwanda vinashiriki operesheni ya kulinda amani, shirika la Human Rights Watch linasema limegunduwa kuwa raia watatu wa Rwanda, akiwemo mkosoaji mmoja maarufu wa utawala wa Kagame, wameuawa ama kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha, huku wengine wakisumbuliwa na maafisa wa ubalozi ama kunusurika majaribio ya mauaji.

Ingawa mashambulizi kama hayo ni machache kwa raia wa Rwanda wanaoishi Ulaya na Marekani, lakini ukweli kwamba yanatokezea kwengineko, unachangia hali ya hofu waliyonayo raia hao hata kama wanaishi maelfu ya kilomita kutoka Rwanda, inasema ripoti hiyo.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW