1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaitaka Rwanda iache ukandamizaji na kuwamata watu

24 Aprili 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch limesema polisi nchini Rwanda wamekamata watu kadhaa tangu amri za kuzuia kuenea kwa COVID-19 kuanza kutekelezwa Machi 22, mwaka huu.

Ruanda Kigali Straße Soldat Wahl 2010
Picha: picture alliance/dpa

Polisi wamekosolewa kwa kukiuka sheria na wakati mwingine kuwakamata watu kwenye viwanja bila kufuata taratibu. 

Shirika hilo limewataka maafisa wa Rwanda kuacha kuwaweka watu kizuizini wakiwemo waandishi habari na wanablogu wanaojaribu kuripoti kuhusu unyanyasaji na kuhakikisha maafisa wa usalama wanazingatia haki za binaadamu wakati wanapotekeleza amri hizo.

Taarifa za mauaji, ubakaji na uhalifu mwingine unaofanywa na maafisa wa usalama wakati huu ambao shughuli za kijamii zimesimamishwa, zinapaswa kuchunguzwa mara moja kwa uwazi na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch Afrika ya Kati, Lewis Mudge amesema maagizo ya serikali kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona hayawapi haki maafisa wa usalama kupuuza utawala wa sheria na kufanya dhulma kwa wananchi, huku wakiwakamata wale wanaojaribu kuripoti kuhusu uhalifu huo.

Watakaokamatwa kufungwa jela au kulipa faini

Tangu amri hizo zianze kutekelezwa, polisi iliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba kushindwa kufuata amri hizo ni kukiuka sheria na imeonya kuwa wale waliokamatwa watalipishwa faini au kufungwa jela. 

Amri hizo ambazo zimeongezwa muda hadi Aprili 30, zinawazuia watu kutembea, ikiwemo kufanya mazoezi, kufunga shule na maeneo ya kuabudia na kupiga marufuku kati ya miji na miji na wilaya pamoja na kufunga mipaka, isipokuwa usafirishaji wa mizigo na bidhaa pamoja na raia wa Rwanda na wakaazi wanaorejea waliokuwa wamewekwa kwenye karantini kwa siku 14. 

Tangu Aprili 8, wanablogu wanne ambao waliripoti kuhusu dhuluma na dereva wa mmoja wa wanablugu hao walikamatwa kwa madai ya kukiuka maagizo ya serikali.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch Afrika ya Kati, Lewis MudgePicha: Human Rights Watch

Katika video iliyochapishwa kwenye televisheni ya mtandaoni ya Ishema Aprili 3, wanawake watatu kutoka eneo linaloitwa Kangondo ya Pili, waliwaambia waandishi habari kwamba wanajeshi wanaofuatilia maagizo hayo, waliwabaka. Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC pia lilitangaza visa vya ubakaji.

Wanawake na wasichana ndiyo wako kwenye hatari kubwa ya unyayasaji wa kijinsia na unyanyasaji mwingine katika wakati huu wa COVID-19. Human Rights Watch imesema maafisa wa Rwanda wanapaswa kuhakikisha kwamba waathirika wa ubakaji wanapatiwa matibabu na msaada wa kisaikolojia.

Jeshi laanzisha uchunguzi

Aprili 4, jeshi la ulinzi la Rwanda lilisema katika taarifa yake kwamba uchunguzi umeanzishwa wa madai hayo ya uhalifu dhidi ya raia kwa wanajeshi kadhaa wasio na nidhamu na watuhumiwa watano wanashikiliwa.

Mudge anasema Aprili 8, Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda, RIB na polisi, walimkamata Valentin Muhirwa na David Byiringiro, wanablogu wawili wanaofanya kazi katika kituo cha televisheni cha Kangondo ya Pili.

Baraza la Habari la Rwanda, lilisema katika taarifa yake ya Aprili 13 waandishi hao hawakukamatwa kutokana na kutekeleza majukumu yao na kwamba waandishi hao hawaruhusiwi kuwahoji wananchi.

Machi 25, vyombo vya habari viliripoti kuwa maafisa wa usalama wa Rwanda waliwaua kwa kuwapiga risasi wakaazi wawili wa wilaya ya Nyanza. Aprili 15, Human Rights Watch iliandika barua kwa Waziri wa Sheria wa Rwanda, Johnson Busingye wakidai kupewa taarifa kuhusu misingi ya kisheria inayosababisha watu hao kukamatwa, lakini hata hivyo barua hiyo haijajibiwa.

(HRW https://bit.ly/2KxEaS4)
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW