1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTunisia

HRW yaitaka Tunisia kuacha kuwafurusha wahamiaji wa Kiafrika

7 Julai 2023

Human Rights Watch yaitaka Tunisia kukoma kuwafurusha wahamiaji wa Kiafrika na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kibinadamu kwa wale ambao serikali iliwapeleka katika eneo hatari la mpaka kati ya Tunisia na Libya.

Tunesien Migranten
Picha: Hasan Mirad/Zumapress/picture alliance

Kundi moja la haki na mbunge kutoka Tunisia, wamesema kuwa serikali ya nchi hiyo imewahamisha mamia ya wahamiaji hao hadi katika eneo hatari la mpakani, huku mashuhuda wakiripoti kuwa watu walipandishwa  treni kuondoka nchini humo kufuatia siku kadhaa za vurugu. Vurugu hizo kati ya wahamiaji na wakaazi ziliendelea kwa wiki moja katika bandari ya Sfax, na raia mmoja kuuawa. Wakaazi walilalamikia tabia isiyofaa ya wahamiaji na wahamiaji nao walilalamikia unyanyasaji wa kibaguzi kutoka kwa wakaazi hao.

Maelfu ya wahamiaji wamiminika katika bandari ya Sfax

Maelfu ya wahamiaji ambao hawajaorodheshwa  wamemiminika katika bandari ya Sfax katika miezi ya hivi karibuni kwa lengo la kuelekea Ulaya kwa kutumia boti zinazoendeshwa na wasafirishaji haramu wa binaadamu, na kusababisha mgogoro wa uhamiaji ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Tunisia.

Wahamiaji waliofurushwa ni kutoka mataifa ya Afrika

Human Rights Watch imesema kuwa watu waliofurushwa ni raia wa mataifa ya Ivory Coast, Cameroon, Mali, Guinea, Chad, Sudan, Senegal na kujumuisha watoto 29 na wanawake watatu wajawazito.

Wahamiaji wa Kiafrika wasubiri treni katika kituo cha SfaxPicha: HOUSSEM ZOUARI/AFP

 

Lauren Seibert, mtafiti wa haki za wakimbizi na wahamiaji katika shirika hilo la haki, amesema sio tu kwamba ni jambo lisilofaa kuwanyanyasa watu na kuwaacha jangwani, lakini pia kwa ujumla suala zima la kuwafukuza ni kukiuka sheria za kimataifa. Hata hivyo, wizara ya masuala ya ndani ya Tunisia haikujibu ombi la kuzungumzia hali hiyo.

Mamia ya wahamiaji wanalala barabarani

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Libya, limesema licha ya changamoto za kufikia eneo hilo, liliweza kutoa msaada wa dharura ya kimatibabu kwa baadhi ya wahamiaji. Mashuhuda wanasema, huku mamlaka ikiwahamisha mamia ya wahamiaji hao karibu na mpaka wa Libya, mamia ya wahamiaji wengi wa Kiafrika walikuwa wanalala barabarani karibu na msikiti wa Lakhmi huko Sfax. Kanda za video zilionesha baadhi ya wakazi wakiwapa wahamiaji hao chakula na maji.

Tunisia yasema haitakuwa mlinzi wa mpaka

Kumekuwa na ongezeko la uhamiaji kuvuka bahari ya Mediterrenia kutoka Tunisia mwaka huu baada ya msako mkali uliofanywa na raia wa nchi hiyo dhidi ya wahamiaji kutoka Kusini mwa jangwa la Sahara wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria huku kukiwa na ripoti za mashambulizi ya kibaguzi. Tunisia inashinikizwa na Ulaya kuzuwia idadi kubwa ya wahamiaji wanaoondokea kutoka maeneo yake ya pwani. Lakini Rais Kais Saied, amesema Tunisia haitakuwa mlinzi wa mpaka na haitakubali kutoa makazi kwa wahamiaji nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW