1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaituhumu Misri kulazimisha kutoweka kwa mwanaharakati

Daniel Gakuba
3 Oktoba 2018

Human Rights Watch imesema polisi ya Misri imelazimisha kutoweka kwa Ghoneim. Shirika hilo la kimataifa limeitaka serikali ya Misri kufafanua alipo mwanasheria huyo mtetezi wa haki za binadamu

Ägypten Präsident al-Sisi
Picha: imago/ZUMA Press/Egyptian President Office

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limeitaka serikali ya Misri kufafanua alipo mwanasheria mtetezi wa haki za binadamu ambaye hajaonekana tangu alipokamatwa.

Tarehe 4 mwezi uliopita wa Septemba, mahakama moja nchini Misri iliamuru kuachiwa huru mwanasheria huyo Ezzat Ghoneim na mwenzake Azzoz Mahgoub wakati uchunguzi dhidi yake ukiendelea, lakini hakuna kilichotokea na wote wawili bado hawajaonekana wala kusikika, tangu Septemba 13.

Human Rights Watch imesema leo hii kuwa polisi ya Misri imelazimisha kutoweka kwa Ghoneim, ambaye alikamatwa mwezi Machi akituhumiwa kupanga njama dhidi ya serikali.

Shirika hilo limemnukuu mke wa Ghoneim, Rasha, ambaye amesema mara ya mwisho alimuona mme wake akizuiliwa katika kituo cha polisi cha al-Haram Kusini mwa mji mkuu Cairo, tarehe 13 Septemba.

Wizara ya mambo ya ndani ya Misri imekataa kutoa taarifa yoyote kuhusu rai hiyo ya Human Rights Watch.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW