HRW yalituhumu jeshi la Burkina Faso kwa kuua makumi ya raia
25 Januari 2024Kulingana na ripoti ya shirika la Human Rights Watch iliyotolewa Alhamisi, maafa hayo yalitokea baada ya mashambulizi matatu ya droni mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita. Mawili katika masoko yaliyojaa watu na jingine katika hafla ya mazishi
Kiongozi wa kijeshi Kapteni Ibrahim Traore, aliyechukua Madaraka baada ya mapinduzimnamo mwaka 2022, amelenga kufanya mashambulizi makali dhidi ya makundi yenye mafungamano na magaidi wa Al-Qaeda na wa kundi linalojiita linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Shirika la Human Rights Watch limesema liliwahoji makumi ya mashuhuda kati ya mwezi Septemba na Novemba na kutathmini picha, kanda za video na vilevile picha za satelaiti.
Jeshi la Burkina Faso lilitumia silaha zenye usahihi mkubwa
Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake makuu mjini New York, imesema jeshi la Burkina Faso lilitumia silaha zake zenye uwezo wa kulenga kwa usahihi, kushambulia mikusanyiko mikubwa ya watu, hivyo kusababisha maafa makubwa miongoni mwa raia. Hatua inayokiuka sheria za vita.
Soma pia: Kikosi cha jeshi chashambuliwa Burkina Faso
Mnamo Agosti 3, kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya Burkina Faso RTB,kiliripoti kuhusu operesheni iliyofaulu ya angani dhidi ya wanamgambo wenye misimamo mikali ya dini ya Kislamu, katika mji wa kaskazini mwa taifa hilo Bouro.
RTB ilionyesha kanda ya video ya shambulizi lililoongozwa likiwapiga makumi ya watu na wanyama kwenye sehemu ya wazi msituni.
Wanajeshi 10 wa Niger wauawa katika shambulio la wanamgambo
Wakaazi wa eneo hilo waliliambia shirika la HRW kwamba watu 28 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye shambulizi lililofanyika katika soko lililojaa watu.
HRW yaitaka Burkina Faso kuwawajibisha wahusika
Manusura watatu walisema wanamgambo walikuwa kwenye pikipiki nne waliingia katika soko moja lililokuwa na takriban mamia ya raia, wakati shambulizi lilipotokea eneo la Bouro.
Mnamo Novemba 18, droni ya jeshi ilishambulia soko jingine lililokuwa na watu wengi katika mpaka wao na Mali karibu na mji wa Boulkessi. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Mali, Niger, Burkina Faso wanakabiliwa na uasi wa jihadi kwa muda mrefu
Human Rights Watch limeiomba serikali ya Burkina Faso kuchunguza mara moja na bila upendeleo kile kinachoonekana kuwa ni uhalifu huo wa kivita, kuwawajibisha wahusika na kuwasaidia wahanga pamoja na familia zao.
Chanzo: AFPE