1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yashutumu unyanyasaji wa mashirika ya kiraia Uganda

Sylvia Mwehozi
27 Agosti 2021

Shirika la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kwamba mamlaka za Uganda mnamo Agosti 20 mwaka huu zilitangaza kuzifunga shughuli za mashirika 54 ya kiraia bila ya kutoa taarifa ya mapema. 

Uganda Kampala Protest
Picha: DW/E. Lubega

Mamlaka ya taifa inayohusika na mashirika yasiyo ya kiserikali ilisema kwamba iliyataarifu mashirika hayo mara baada ya kusitisha shughuli zake. Wafanyakazi katika baadhi ya asasi hizo wamelieleza shirika la Human Rights watch kwamba taarifa hiyo iliwafikia saa au siku chache baadae, wakitaka serikali ibatilishe uamuzi wake.

Mkurugenzi wa mamlaka ya Uganda Stephen Okello alisema kwamba mashirika 23 yaligundulika kuendesha shughuli zake wakati vibali vyao vikiwa vimemalizika na asasi 15 "mara kwa mara zilishindwa kutoa malipo ya kila mwaka na vitabu vya mahesabu yaliyokaguliwa". Mashirika mengine 16 yalidaiwa kuendesha shughuli zake kama asasi zisizo za kiserikali bila ya kusajiliwa.

Baadhi ya wafanyakazi wa asasi hizo za kiraia wameelezea wasiwasi juu ya mamlaka kushindwa kuwapatia nafasi ya kujibu madai hayo kabla ya kuchukua hatua kali kama hizo. Mtafiti wa Human Rights Watch kanda ya Afrika Oryem Nyeko alisema hatua hizo kwa mara nyingine namna zinavyoyapuuza mashirika ya kiraia.

Godber Tumushabe, mkurugenzi wa shirika la kituo cha masomo ya kimkakati katika eneo la maziwa makuu GLISS alilieleza shirika la Human Rights Watch kwamba alipokea barua kutoka kwa serikali ikimueleza kwamba shughuli za asasi yake zimesitishwa kwasababu shirika lake halikuwa limesajiliwa. Tumushabe hata hivyo anadai kwamba shirika lake limesajiliwa ingawa anaamini kwamba lililengwa kwasababu ya historia yake ya nyuma alipofanya kazi kama mwanaharakati.

Polisi wa Uganda wakihangaika na mfuasi wa upinzaniPicha: Reuters/G. Tomasevic

Kwa muda mrefu mamlaka nchini humo zimeshindwa kuchunguza wimbi la wizi na mashambulizi dhidi ya ofisi za mashirika makubwa ya kiraia katika miaka ya hivi karibuni. Mei 2016, watu wasiofahamika walivunja na kuingia katika asasi moja ya ulinzi wa haki za binadamu ya Uganda HRAPF, wakimpiga vibaya mlinzi na kuiba nyaraka. Ofisi hizo zilivamiwa tena Februari 8 mwaka 2018 lakini tangu wakati huo hakuna uchunguzi uliofanyika.

Mwaka 2019 mamlaka zilipiga marufuku shirika la muungano wa kiraia wa demokrasia ya uchaguzi nchini Uganda CCEDU kujihusisha na elimu ya mpiga kura au shughuli yoyote inayohusiana na uchaguzi. Mwaka huu mnamo wezi Januari shirika jingine la uangalizi wa uchaguzi Uganda nalo lilifungiwa. Siku ya uchaguzi polisi waliwakamata watu zaidi ya 20 kutoka mashirika mbalimbali ya kiraia.

Human Rights Watch imetoa mwito wa serikali kuweka mazingira rafiki kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuendesha shughuli zake na kuhakikisha kwamba uamuzi wowote ambao unaathiri shughuli za mashirika hayo unapaswa kufuata mchakato sahihi, ikiwemo kuyapatia taarifa ya mapema na kuyaruhusu mashirika yaliyoathirika kukata rufaa kwa ajili ya maamuzi hayo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW