1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yataka Burundi imuachie Nibitanga

13 Desemba 2017

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitaka serikali ya Burundi kumuachia ama kumfikisha mahakamani haraka mwanaharakati wa haki za binaadamu, Nestor Nibitanga, anayeshikiliwa tangu Novemba 21.

Protest in Burundi gegen UN-Bericht
Picha: picture-alliance/AA/R. Ndabashinze

Ripoti ya shirika hilo iliyotolewa leo (Disemba 13) inasema kuwa Nibitanga alikamatwa kwa tuhuma za "kutishia usalama wa taifa" kwa mujibu wa tamko la polisi kupitia mtandao wa Twitter.

Mwanaharakati huyo alikamatwa nyumbani kwake katika jimbo la Gitenga na kupelekwa kwenye makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa (SNR) mjini Bujumbura, ambako "lishikiliwa bila kuruhusiwa kuwasiliana na familia wala wakili wake hadi tarehe 4 Disemba alipopelekwa jela la Rumonge kusini mwa Bujumbura, aliko hadi sasa."

"Kukamatwa kwa Nibitanga ni tukio la hivi karibuni kabisa katika mkururo wa hatua za kikandamizaji dhidi ya watetezi huru wa haki za binaadamu na waandishi wa habari nchini Burundi," alisema Ida Sawyer, mkurugenzi wa HRW kwenye eneo la Afrika ya Kati. 

Kwa mujibu wa Sawyer, kukamatwa huku kwa Nibitanga kunatuma ujumbe kwa wanaharakati na waandishi wachache waliobakia ndani ya nchi kwamba "wanapaswa kubakia kimya."

Nibitanga alikuwa muangalizi wa Shirika la Ulinzi wa Haki za Binaadamu na Mahabusu (APRODH) kwenye maeneo ya kati na mashariki mwa Burundi. Miongoni mwa majukumu yake yalikuwa ni kukusanya taarifa za uvunjaji wa haki za binaadamu katika majimbo ya Gitega, Cankuzo, Ruyigi na Karuzi. Pia alikuwa akitembelea vituo wanamoshikiliwa mahabusu. 

Taasisi yake ya APRODH ilikuwa ndiyo kubwa kabisa ya kufuatilia masuala ya haki za binaadamu kabla ya kufungiwa na serikali mnamo Oktoba 2016. 

Kamatakamata dhidi ya watetezi wa haki za binaadamu zashamiri

HRW imekusanya ushahidi wa matukio ya kuteswa na kudhalilishwa kwa wanaharakati na waandishi kadhaa nchini Burundi katika siku za karibuni. Miongoni mwao ni wale walioshikiliwa kwenye makao makuu ya SNR, ambapo wanasema maafisa wa Idara hiyo ya Usalama wa Taifa wanawapiga wafuasi wa upinzani kwa nyundo na nondo, kuwakata kwa vyuma miguuni, kuwamwagia plastiki iliyeyushwa kwa moto, kuwabana korodani na kuwapiga shoti za umeme.

Tangu Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania na kushinda muhula wa tatu wenye utata, kumekuwa na matukio kadhaa ya kukamatwa na kuteswa kwa wakosoaji, wapinzani na watetezi wa haki za binaadamu pamoja na waandishi wa habari.Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Kukamatwa kwa Nibitanga kunafuatia kukamatwa kwa Germain Rukuki, mjumbe wa zamani wa Shirika la Wakristo Wapingao Mateso nchini Burundi (ACAT-Burundi) mnamo Julai 2017. Kama APRODH, shirika hili nalo lilifungiwa mwezi Oktoba 2016 na kama Nibitanga, Rukuki pia alishikiliwa kwanza kwenye mahabusu ya SNR kabla ya kupelekwa jela ya Ngozi.

Baadaye alituhumiwa kwa "kuhatarisha usalama wa taifa" na "uasi", kabla ya kukataliwa dhamana na kusalia kwenye jela hiyo hadi leo akisubiri kesi dhidi yake.

Kamamatakamata hizi za karibuni zinafuatia mkururuo wa matukio ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani, wakosoaji, waandishi wa habari na watetezi wa haki za binaadamu tangu mwaka 2015, baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania muhula mwengine wa tatu wenye utata. 

Tangu wakati huo, watetezi na waandishi wa habari wengi maarufu wameikimbia nchi hiyo kwa usalama wao. Mnamo mwezi Agosti 2015, rais wa APRODH, Pierre Claver Mbonimpa, alipigwa risasi usoni na shingoni na mtu asiyejuilikana wakati akielekea nyumbani kwake kutoka kazini.

Mbonimpa aliwahi kukamatwa mwezi Mei 2014 na kushitakiwa kwa kuhatarisha usalama wa taifa kutokana na kauli aliyotoa redioni. Baada ya kuumwa sana, aliachiwa kwa muda kwa sababu za kiafya, lakini mashitaka dhidi yake hayakufutwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/HRW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman