HRW yataka UN kulichunguza jeshi la Ethiopia kwa mauaji
4 Aprili 2024Tume ya Haki za Binaadamu ya Ethiopia, ambayo ni taasisi huru ya umma, ilikadiria mwezi Februari kuwa karibu watu 45 waliuliwa mnamo Januari 29 na vikosi vya serikali katika mji wa Merawi baada ya kuzuka makabiliano na wapiganaji wa eneo hilo wanaofahamika kama Fano.
Soma pia: Watu 400 wafa njaa mikoa ya Tigray na Amhara
Kwa mujibu wa ushuhuda uliokusanywa na shirika hilo la haki lenye makao makuu yake mjini New York Marekani, baada ya kundi la Fano kujiondoa kutoka Merawi, wanajeshi wa Ethiopia waliwapiga risasi raia mitaani Pamoja na wakati wa uvamizi wa majumbani kwa kipindi cha saa sita.
HRW imemhimiza Kamishena wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi huru kuhusu ukiukaji unaofanywa katika mkoa huo.
Shirika hilo lisilo la kiserikali limeutaka Umoja wa Afrika kusitisha uchangiaji wa vikosi vya serikali ya shirikisho ya Ethiopia katika operesheni za kulinda amani hadi pale makamanda wanaohusika na ukiukaji huo mkubwa wa haki watakapowajibishwa.
Soma pia: Abiy Ahmed akanusha watu kufa kwa njaa Ethiopia
Mnamo Februari 24, askari wa Ethiopia waliwauwa kiholela karibu raia wanane mjini Merawi kufuatia shambulizi jingine la wapiganaji wa Fano mjini humo. Kando na kuwahoji waathirika, HRW pia ilizichunguza video mbili zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya shambulizi la Januari 29, na kutumia picha za satelaiti kubainisha ukweli. Baada ya kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wake kwa serikali, hawakupewa jibu lolote.
Washirika wa kimataifa wa Ethiopia, zikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya, na Uingereza, walitoa taarifa wakilaani mauaji hayo ya kikatili ya raia na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi huru.
Chini ya sheria za kimataifa za ubinaadamu zinazotumika kwa mgogoro wa Amhara, matukio ya mauaji ya makusudi au kuteswa kwa raia, na kupora na kuteketeza mali za raia yamepigwa marufuku na yanaweza kushitakiwa kama uhalifu wa kivita.
Msemaji wa serikali ya Ethiopia aliviambia vyombo vya habari kuwa wapiganaji wa Fano waliishambulia kambi ya jeshi ya Merawi lakini akasisitiza kuwa jeshi lilichukua tu hatua ya kujilinda, ikiwa ni pamoja na wakati walipofanya upekuzi majumbani, na halikuwalenga raia. Wakaazi walisema wanajeshi wa Ethiopia waliitisha kikao Februari 12 na hapo ndipo walikiri kuwa raia wanne waliuawa na kuwa ni bajaji moja tu iliyochomwa moto.
Mapema Februari, bunge la Ethiopia lilirefusha hali ya hatari iliyowekwa Agosti 2023 katika jimbo la Amhara – ambalo ni la pili kwa idadi kubwa ya watu nchini Ethiopia – katika jaribio ambalo halijafua dafu la kutuliza uasi wa kundi la Fano.
Wapiganaji wa Fano na Amhara wanahisi kusalitiwa na makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka wa 2022 na serikali na viongozi wa waasi wa mkoa wa Tigray.