HRW yaitaka Tunisia kuacha kuwafurusha wahamiaji wa Kiafrika
7 Julai 2023Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake mjini New York, Human Rights Watch, limeitaka serikali ya Tunisia kusitisha hatua ya kuwafukuza wahamiaji wanaotoka kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika kutoka nchini humo.
Shirika hilo linataka pia Tunisia iwezeshe huduma za kiutu kuwafikia wahamiaji ambao iliwapeleka sehemu iliyo hatari katika mpaka wa Tunisia na Libya. Hapo Jumatano, shirika moja la haki za binadamu nchini Tunisia pamoja na mbunge, walisema nchi hiyo imewapeleka mamia ya wahamiaji katika eneo hilo lililo mpakani.
Kumekuwa na msuguano kati ya wahamiaji na wakaazi katika bandari ya Sfax na Mtunisia mmoja aliuwawa. Wakaazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamikia usumbufu wa wahamiaji huku wahamiaji nao wakilalamikia kubaguliwa kutokana na rangi zao.