HRW yaitaka UN kuwalinda raia wenye njaa Sudan
30 Agosti 2025
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuchukua hatua za haraka kuwalinda raia katika maeneo ya Magharibi mwa Sudan dhidi ya mashambulizi haramu na njaa.
Shirika hilo limelitaka Baraza hilo lishinikize kundi la waasi la Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kusitisha mashambulizi dhidi ya raia, ikiwemo kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, na kuzitaka pande zote mbili zinazopigana kusitisha kuzuia njia za misaada ya kibinadamu.
Pia, shirika la Human Rights Watch linataka kuongezwa kwa vikwazo vya silaha kwa Darfur na katika nchi nzima, na viongozi wa pande zinazopigana, hasa wa kundi la RSF, wawekwe chini ya vikwazo kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Tangu Aprili 2024, wapiganaji wa kundi la RSF wameuzingira mji wa El Fasher, hali ambayo imezuia misaada ya kibinadamu na bidhaa muhimu. Mashambulizi ya wapiganaji wa RSF yameua raia wengi, hasa katika kambi ya Abu Shouk, limesema shirika la HRW katika taarifa yake.
Misaada yazuiwa kuingizwa El-Fasher
Mnamo Agosti 11, kundi la RSF lilishambulia tena kambi hiyo, na kuua angalau raia 57. Watu waliokimbia wamesimulia mateso, ubakaji, uporaji, na mashambulizi ya mabomu.
Baraza la Usalama lilitoa tamko la kulaani mashambulizi hayo mnamo Agosti 13, lakini halikuchukua hatua madhubuti dhidi ya wahusika. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilionya kuwa halijaweza kufikisha misaada El Fasher kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku wakazi wakilazimika kula chakula cha mifugo.
Katika maeneo ya Kordofan, mashambulizi ya anga ya Jeshi la Sudan (SAF) yameua raia na kuharibu miundombinu ya kiraia. Kundi la RSF pia limeshambulia vijiji kadhaa, na kuua zaidi ya watu 300, wakiwemo watoto na wanawake wajawazito, inaelezea ripoti ya shirika la HRW. Ripoti zinaonyesha kuwa kundi la RSF na washirika wao wamewalenga jamii zisizo za Kiarabu, hasa Wazaghawa.
"Raia wa Darfur Kaskazini wamekumbwa na njaa na mashambulizi ya makusudi"
Shirika la kutetea haki za binadamu la HRW linalitaka Baraza la Usalama lifanye tathmini ya hatua zilizochukuliwa tangu ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ya Oktoba 2024 kuhusu ulinzi wa raia, na kuzingatia uwezekano wa kupeleka kikosi cha kulinda raia Sudan.
"Kwa zaidi ya mwaka mmoja, raia wa Darfur Kaskazini wamekumbwa na njaa na mashambulizi ya makusudi, huku ghasia zikiongezeka Kordofan,” amesema Laetitia Bader wa shirika la HRW. "Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua madhubuti, zenye muda maalum, ikiwemo vikwazo vya moja kwa moja dhidi ya wahusika", alisisitiza Bi Bader.
Mzozo wa sasa wa Sudan kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ulianza rasmi tarehe 15 Aprili 2023.
Tangu wakati huo, mapigano yameenea katika maeneo mbalimbali ya nchi, yakiathiri mamilioni ya raia, kusababisha vifo, uharibifu wa miundombinu, na janga kubwa la kibinadamu. Mzozo huu umetokana na mvutano wa muda mrefu kuhusu mamlaka ya kisiasa na kijeshi baada ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Omar al-Bashir mwaka 2019.