1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiUrusi

HRW:Sheria ya Urusi inazuia shughuli za mashirika ya kigeni

5 Agosti 2023

Shirika la Human Rights Watch limesema hatua ya Bunge la Urusi kupitisha mswada unaokataza ushirikiano na mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali ambayo hayajasajiliwa, kutazuia shughuli za kiraia.

Human Rights Watch | Logo
Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Shirika hilo la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema sheria hiyo itakandamiza kwa kiasi kikubwa haki ya uhuru wa kujumuika inayolindwa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu ikiwa utaidhinishwa na Bunge na kutiwa saini na Rais Putin.

Mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za makosa ya Jinai, ambayo yatatoa adhabu kwa mtu yeyote atakayeshiriki katika shughuli za shirika la kigeni lisilo la kiserikali na ambalo halijasajiliwa nchini Urusi atakabiliwa na faini ya hadi dola 55 kwa kosa la kwanza.

Makosa matatu  ndani ya mwaka mmoja yatapelekea mhusika kufunguliwa mashitaka ya jinai na uwezekano wa kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka miwili jela.

Kosa la kuandaa shughuli za kikundi cha kigeni ambacho hakijasajiliwa, litaadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela. Mswada huo pia utaziruhusu mamlaka kuwafurusha nchini Urusi, raia wa kigeni ambao hatofuata sheria.

Mashirika ya kiraia yakosoa hatua hiyo

Bunge la Urusi Picha: The State Duma/AP/picture alliance

Tanya Lokshina, mkurugenzi mwenza anayehusika na eneo la Ulaya na Asia ya Kati katika shirika la Human Rights Watch amesema sheria hii ya kupiga marufuku ushirikiano na mashirika huru ya kigeni ni hatua nyingine kubwa katika kampeni ya serikali ya Urusi ya kuzifurusha jumuiya za kiraia.

Ameendelea kuwa hatua hii inalenga kuwatenga zaidi wanaharakati wa Urusi na wenzao wa kimataifa na hivyo kuwaacha bila msaada wowote katika mazingira yanayozidi kuwa ya uhasama.

Soma pia: Viongozi wa Baraza la Haki la Ulaya waungana dhidi ya Urusi

Katika miaka ya hivi karibuni, wanahabari wengi wa Urusi, watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wa mashirika ya kiraia wameikimbia nchi kwa kuhofia kufunguliwa mashtaka ya uhalifu yaliyochochewa kisiasa.

Idadi ya walioihama Urusi imekuwa kubwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kupasishwa kwa sheria kali za kudhibiti taarifa zinazohusiana na vita. Hata hivyo, wanaharakati wengi walichagua kubaki nchini humo licha ya hatari kubwa inayowakabili. Watu hao waliendelea na shughuli zao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na washirika wa kigeni ambao usajili wao ulisitishwa na mamlaka za Moscow.

Wanaounga mkono sheria hiyo wajieleza

Amnesty International ni mojawapo ya mashirika ya kigeni yaliyolengwa na sheria hiyoPicha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Mmoja wa wanaounga mkono marufuku hiyo, Sergey Leonov wa chama cha Liberal Democratic amesema lengo la sheria hiyo mpya ni kukabiliana na harakati za makundi ya kigeni zinazolenga kuathiri maslahi ya Urusi.

Mnamo Aprili 8, 2022, Wizara ya sheria ilibatilisha usajili wa shirika la Human Rights Watch, ambalo lilidumisha ofisi yake nchini Urusi kwa miaka 30, pamoja na Amnesty International na mashirika mengine ya kigeni 13 yasiyo ya kiserikali. Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, wizara hiyo ilitoa sababu ya ukiukaji wa sheria za Urusi bila hata hivyo kutoa ufafanuzi zaidi.

Amnesty: Urusi imefanya uhalifu Ukraine

01:01

This browser does not support the video element.

Marufuku hii mpya inatokana na sheria ya mwaka 2015 inayolenga kile kinachoitwa "mashirika yasiyofaa," ambayo inampa mwendesha mashtaka mkuu mamlaka isiyo na kizuizi ya kupiga marufuku mashirika ya kigeni ambayo yanaonekana kuwa tishio kwa utaratibu wa kikatiba au usalama wa Urusi.

Soma pia:Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine

Orodha ya "mashirika hayo yasiyotakiwa" kwa sasa inajumuisha mashirika karibu 93 ikiwemo Transparency International, Greenpeace International, na Human Rights House Foundation.

Kujihusisha na shirika la kigeni "lisilotakiwa" kunaadhibiwa kwa faini ya hadi dola za Marekani 166 kwa kosa la kwanza na hadi miaka minne jela unaporudia kosa hilo. Kuongoza shirika "lisilohitajika" kunaweza kupelekea adhabu ya hadi miaka sita jela.

Rais wa Urusi Vladimir Putin- anatarajia kutia saini muswada huoPicha: Sergei Bobylyov/TASS/REUTERS

Wanaharakati watatu wa Urusi tayari wamehukumiwa vifungo kwa madai ya ukiukaji wa sheria hii juu ya " mashirika yasiyotakiwa." Marufuku hii mpya pia itaimarisha pia sheria ya "mawakala wa kigeni", ambayo kwa muda mrefu imekuwa chombo muhimu cha Ikulu ya Kremlin katika ukandamizaji wa mashirika ya kiraia.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wahofia ukiukaji wa haki unaofanywa na Urusi, Ukraine

Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE), Tume ya Ulaya ya Demokrasia na Sheria na wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wote wameikosoa sheria hii mpya ya Urusi.

Chanzo: (HRW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW