1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW:Waliofukuzwa Saudia wanashikiliwa na kuteswa Ethiopia

Angela Mdungu
5 Januari 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo kuwa, mamlaka za Ethiopia zimewakamata kiholela, na kuwatesa maelfu ya watu wa Tigray waliorejea nchini humo baada ya kufukuzwa nchini Saudi Arabia

Saudi Arabien I Äthiopische Migranten werden in ihr Herkunftsland zurückgebracht
Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Mamlaka za Ethiopia zimewakamata na kuwahamisha kwa nguvu Watigray waliofukuzwa Saudi Arabia na kuwaweka katika vituo vilivyo kwenye mji mkuu, Addis Ababa ambako baadhi yao wanashikiliwa kinyume cha sheria.  

Watu hao pia wamekuwa wakikamatwa katika vituo vya ukaguzi kwenye barabara za kuelekea Tigray na uwanja wa ndege wa Semera katika mkoa wa Afar na kupelekwa vizuizini huko huko Afar na kusini mwa Ethiopia. 

Ripoti ya shirika la Human Rights Watch imesema Saudi Arabia inapaswa kuacha kuendelea kuwaweka wahamiaji wa Tigray katika mazingira magumu na kuwarudisha Ethiopia

Mtafiti wa masuala ya haki za wakimbizi na wahamiaji wa shirika hilo la  Nadia Hardman amesema  Saudi Arabia inapaswa kuwapa ulinzi watu wa Tigray walio hatarini na kwamba Ethiopia inapaswa kuwaachilia wale wote waliofukuzwa kutoka Saudia.

Ripoti ya Human rights Watch, imesema baadhi ya wahamiaji hao iliyowahoji wameeleza kwamba wakiwa kwenye vituo wanavyoshikiliwa mwanzoni walipewa uhuru wa kuzunguka ndani ya vituo vya mjini Adis Abbaba lakini walikataliwa kutoka kwenda nyumbani. Wengine kati ya hao waliojaribu kutafuta njia ya kuondoka walikamatwa na kuondolewa kwa nguvu kwenye vituo vya awali na kupelekwa kwenye vizuizi vya mkoa wa Afar ambako polisi waliwapiga au kuwatesa kwa kutumia mipira na bakora.

Wengi wa waliohojiwa wamesema hawakuweza kuzungumza na familia zao kuwajulisha mahali walipokuwa huku baadhi ya familia zikiamini kuwa bado walikuwa Saudia.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed AliPicha: Office of the Prime Minister Ethiopia/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Human Rights Watch limesema hatua ya mamlaka za Ethiopia kuwashikilia maelfu ya watu hao bila kuzifahamisha familia zao inakiuka sheria za kimataifa. Limeitaka serikali ya nchi hiyo kuwaachilia wale wote ambao hawajafunguliwa mashtaka na kuongeza kuwa wote wanaoshikiliwa wanapaswa kupata huduma za kisheria na kuwasiliana na familia zao

Sababu mbalimbali, zikiwemo ukosefu wa ajira na changamoto nyingine za kiuchumi ukame, na ukiukwaji wa haki za binadamu zimewafanya mamia kwa maelfu ya raia wa Ethiopia wahyahame makazi yao wakisafiri kwa mashua katika bahari ya shamu na kisha kwa njia ya nchi kavu kupitia Yemen wakielekea Saudia kwa takribani muongo mmoja sasa.