1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huawei yaapa kusonga mbele na 5G

19 Desemba 2019

Licha ya Rais Trump wa Marekani kuitangaza kampuni ya Huawei ya China kuwa hatari, mwenyekiti wa kampuni hiyo Liang Hua anasema kipaumbele chao pekee ni kuendelea kudumu kwenye kilele cha teknolojia.

Interview Huawei Chairman Liang Hua
Picha: DW

Majengo ya kampuni kubwa ya teknolojia ya China, Huawei, kusini mwa mji wa Shenzhen yamezungukwa na miti na vijibwawa vidogo vidogo. Wafanyakazi vijana wanapita huku na kule wakiwa wamevalia suruali za jinzi, fulana na viatu vya raba.

Wakati wa chakula cha mchana, watu hupata usingizi kwenye magodoro ya kukunja.

Mazingira ni ya utulivu hapa, na mtu hawezi kujuwa kuwa yupo kwenye kampuni ambayo imekumbwa na ushindani wa kilimwengu kwenye mawasiliano ya kisasa.

Huawei, hapana shaka yoyote, ndiyo inayoongoza ulimwenguni kwenye teknolojia ya data iitwayo "Kizazi cha Tano cha Mawasiliano ya Mtandaoni" au 5G, ambayo inatazamiwa kuhusisha kila kitu, kutoka gari na viwanda hadi miji na ulimwengu wote wa mtandaoni.

Kampuni hii pia ndiyo kubwa kabisa ulimwengunji kujenga miundombinu inayowezesha mtandao huo wa 5G kufanya kazi. Na hilo ni jambo ambalo mwenyekiti wa kampuni hiyo, Liang Hua, analionea fahari sana.

"Kuhusiana na 5G, hivi sasa ulimwengu unazidi kuweka msisitizo wake kwenye hili. Upotoshaji wa Marekani umesaidia. Ukweli ni kuwa Huawei inaongoza kwa 5G kwa kuwa tulianza kuwekeza mapema, na hilo likatupa nafasi ya juu kwenye ushindani kwenye teknolojia, bidhaa na miundo ya 5G," anasema Liang.

Marekani yazidi kuiandama Huawei

Hata hivyo, Huawei imejikuta ikilazimika kujitetea kila mara tangu Marekani, chini ya Rais Donald Trump, kuishutumu kampuni hiyo kwa kutishia usalama wa taifa.

Liang Hua, mwenyekiti wa kampuni ya teknolojia ya China, Huawei.Picha: DW/Jun Yan

Serikali ya Marekani inadai kuwa Huawei inaweza kutumika kuwezesha ujasusi wa chama cha Kikomunisti cha China na mwezi Mei 2019, ikazipiga marufuku kampuni za Kimarekani kufanya kazi na Huawei bila kibali maalum.

Baada ya hatua hiyo, mwanzilishi wa Huawei, Ren Zhengfei alisema kampuni hiyo ya Kichina imekuwa kama ndege inayoshambuliwa vikali ikiwa angani, na Liang Hua anasema hilo ni kweli.

"Naam, nakubaliana naye. Ndege anayoitaja kwenye taswira hii inaendelea kuruka hata baada ya kutobolewa kwa risasi, na hatimaye inarejea salama nyumbani. Huawei tumekuwa kama ndege hiyo baada ya kuorodheshwa kwenye vikwazo vya serikali ya Marekani. Ili kutuwa salama, tulipaswa kutatua matatizo kadhaa na kuliziba kila tobo, kama vile kuzitengeneza upya baadhi ya bidhaa zetu na kuhakikisha uzalishaji na usambazaji unaendelea."

Kwa mujibu wa Liang, lengo kuu la Huawei ni kuendelea kudumu kwenye sekta hii ya teknolojia, ingawa njia ya kufika huko si rahisi.

Kwenye tafrija waliyoiisha mwezi Juni mwaka huu, mwanzilishi wa Huawei, Ren, alisema kuwa kampuni yao inatazamiwa kushuka kwa dola bilioni 30 ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW