1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu Afghanistan zitakutana Doha kwa mazungumzo

7 Septemba 2020

Afisa mmoja wa serikali ya Afghanistan amesema wapatanishi wa upande wa serikali nchini humo wanatarajiwa kushinikiza usitishwaji wa mapigano wakati wa mazungumzo yao na kundi la Taliban mjini Doha.

Afghanistan Kabul | Ashraf Ghani, Sarwar Danish und Amrullah Saleh
Picha: Getty Images/AFP/W. Kohsar

Tarehe kamili ya mazungumzo hayo yatakayofanyika katika mji mkuu wa Qatar Doha, bado haijatajwa lakini pande zote mbili zimekubali kuwa mazungumzo hayo huenda yakaanza hivi karibuni baada ya hatua iliyokuwa na utata ya kubadilishana wafungwa kukamilika wiki iliyopita. 

Kulingana na makamu wa rais wa Afghanistan Amrullah Saleh, nia ya kweli ya Taliban itajulikana wazi katika mazungumzo hayo wakati upande wa serikali utakapowasilisha hoja ya kusitisha mapigano. Amesema huo ndio utakuwa mtihani wa kwanza kwa kundi hilo na watakapolikubali hilo, itaonesha kuwa wana dhamira ya kweli ya amani ya taifa hilo. 

Amrullah Saleh amesema ujumbe wa Afghanistan utaelekea Doha wakati masuala yote yanayohusiana na safari hiyo yatakapokamilika. Hata hivyo amesema upande wa serikali hautakubali kuwekewa shinikizo.

Suala la ubadilishanaji wa wafungwa lilisababisha mkutano kucheleweshwa

Baadhi ya wafungwa kutoka upande wa Taliban Picha: Reuters/National Security Council of Afghanistan

Mazungumzo hayo yalitarajiwa kuanza mwezi Machi kama ilivyokubalika katika mkutano kati ya Taliban na wajumbe kutoka Marekani mwezi Februari mwaka huu.  Lakini tofauti zilizojitokeza kuhusianan na suala hilo la ubasilishanaji wafungwa ndilo lililochelewesha kupanga tarehe ya mazungumzo kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban. 

Kulingana na mpango wa Marekani na Taliban, Serikali ya Afghanistan ilipaswa kuwaachia huru wanamgambo 5000 ili kundi hilo nalo liwaachie huru wanajeshi 1000 kutoka Afhhanistan. Mpango huo ulikamilika wili iliyopita isipokuwa kuachiwa kwa wanamgambo kadhaa kulikopingwa na Ufaransa pamoja na Australia.

Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa kundi la TalibanSuhail Shaheen amesema wajumbe wa kundi hilo wameshawawili nchini Qatar. Akizungumza na shirika la habari la AFP Shaheen amesema wajumbe wote wamefika kwa mazungumzo na yataanza baada ya masuala kadhaa kusuluhishwa.

Mjumbe maalum wa Marekani kwa Afghanstan anayeratibu makubaliano kati ya serikali na kundi la Taliban Zalmay Khalilzad yupo tayari mjini Doha, hatua inayoashirikia mazungumzo hayo kweli huenda yakaanza hivi karibuni. 

Taarifa kutoka serikali ya Marekani imesema watu wa Afghanistan wako tayari kupunguza machafuko nchini mwao na kutafuta suluhu la kisiasa kumaliza kabisa vita nchini humo na kwamba viongozi wa Afghanistan wanapaswa kuchukua nafasi hii kutafuta amani ya nchi yao. 

Chanzo: afp.reuters, ap