Hujuma za makombora dhidi ya Syria Magazetini
16 Aprili 2018
Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Miaka saba baada ya vita kuripuka nchini Syria na kuyahusisha madola yote makubwa, hujuma hizi mpya za makombora zingekuwa za maana kama zingefuatiwa haraka na juhudi mpya na za dhati za amani. Haitoshi kwa dola kubwa kama Marekani, kujikita katika kulipiza kisasi tu na janga linalozidi kukua kuyaachia mataifa mfano wa Iran, Urusi na Saudi Arabia."
Wananchi wanataka kujua ukweli
Baadhi ya wahariri wanazungumzia shinikizo linalowakumba viongozi wa Uingereza na Ufaransa waliojiunga na rais Donald Trump katika kuishambulia Syria. Wanakumbusha hoja zilizotolewa na Marekani kabla ya kuishambulia Iraq mwaka 2003. Mhariri wa gazeti la "Freie Presse" anaandika: "Uwongo ni kitu cha kawaida katika vita. Lakini katika mataifa ya kidemokrasi ya magharibi shinikizo la wananchi wao kuhusu uhalali wa vita ni kubwa zaidi kuliko katika nchi za utawala wa kiimla. Na hasa tangu vita vya Iraq vilivyoanzishwa kwa msingi wa ripoti za uwongo mkubwa, hakuna anaesubuutu kuwapa uso wananchi na kuwasihi wawaamini, kwa sababu wanachofanya ni cha maana. Imani kama hiyo inahitaji ushahidi. Ufaransa inaposema inataka tume huru iundwe kuchunguza yaliyotokea Duma, ni sawa lakini mpangilio haufuatani. Kutumiwa gesi za sumu dhidi ya raia ni uhalifu wa vita ambapo unabidi uchunguzwe na kuadhibiwa. Matumizi ya nguvu dhidi ya vituo vinavyotengeneza sumu hizo na pia dhidi ya nguvu za kijeshi yanaweza kuwa hatua ya mwisho ikiwa hakuna njia nyengine. Lakini ni hatua zilizokuwa zichukuliwe baada ya uchunguzi na sio kufuatia dhana.
Balaa kubwa limeepukwa
Gazeti la mjini Freiburg, "Badische Zeitung" linashukuru kwamba hujuma zilizoongozwa na Marekani na kuungwa mkono na Ufaransa na Uingereza hazikuzusha balaa kubwa zaidi dhidi ya Urusi. Gazeti linaendelea kuandika: "Yeyote yule aliyejionea picha za jinsi wahanga wa mashambulio ya gesi za sumu Ghuta ya mashariki walivyokuwa wakiteseka, basi hatokosa kuzitaja hujuma za makombora ya Marekani, Ufaransa na Uingereza kuwa ni hadaa. Licha ya risala kali kali za rais wa Marekani Donald Trump kupitia mtandao wa Twitter, nchi shirika zimefanya mashambulio ya kijuu juu tuu. Lakini kwa kuwa hayakuwa mashambulio makali basi mtu anaweza kusema ulikuwa ushindi wa wenye busara. Balaa la kuripuka mapigano pamoja na Urusi katika ardhi ya Syria na kutishia ulimwengu mzima limeweza kuepukwa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse
Mhariri:Josephat Charo