1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Hujuma za RSF zasababisha kufungwa hospitali muhimu Sudan

Hawa Bihoga
10 Juni 2024

Hospitali pekee ambayo ilikuwa ikitoa huduma katika mji wa kimkakati wa El-Fasher nchini Sudan imefungwa baada ya shambulio la wanamgambo wa Kikosi cha Dharura, RSF, waliojaribu kuuteka mji huo.

Darfur, El Fasher, Sudan | MSF | Wagonjwa wakiwa wamerundikana wakisubiri matibabu.
Wagonjwa wakiwa wamejazana katika hospitali muhimu El Fasher.Picha: ALI SHUKUR/AFP

Shirika la kimataifa la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema kuwa wanamgambo wa RSF waliishambulia hospitali hiyo iliyo kusini mwa mji wa El-Fasher, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, mwishoni mwa juma na kuwafyatulia risasi wahudumu wa afya na wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu hospitalini hapo.

Kupitia tamko la pamoja kati ya wizara ya afya Sudan na MSF lililochapishwa katika mtandao wa X, wamesema kuwa siku ya Jumamosi walifikia uamuzi wa kusimamisha utoaji wa huduma katika hospitali hiyo, kufuatia uvamizi uliofanywa na wanamgambo wa RSF uliokwenda sambamba na uporaji na kuibwa kwa gari, mali ya shirika hilo la hisani.

Soma pia:Jeshi la Sudan laapa ''kujibu vikali' shambulizi la RSF

Mji huo wa El-Fasher ulikuwa unashuhudia mapigano ya hapa na pale tangu vita vilipozuka mwezi wa Aprili 2023, lakini mapigano makali na mabaya yalizuka mnamo  Mei 10 katika kile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekiita "sura mpya ya kutisha" katika mzozo huo.

Kulingana na MSF tangu wakati huo takriban watu 192 wameuwawa na wengine zaidi ya 1,230 wamejeruhiwa katika mji huoz.

Ikumbukwe kwamba mji huo, umekuwa kimbilio kwa Wasudan wengi wanaokimbia mapigano lakini pia uko kwenye ukingo wa kutumbukia katika baa la njaa kutokana na misaada ya kiutu kutofika kwa wakati, hii ni kulingana na mshirika ya kutoa misaada ikiwemo yale ya Umoja wa Mataifa.

Mji wa El-Fasher ambao upo Darfur Kaskazini ni mji pekee ambao haupo chini ya udhibiti wa wanamgambo wa RFS kwenye eneo hilo na ni kituo muhimu cha kujihifadhi waathirika wa mzozo huo.

Sudan katika kulinda udhibiti wa El-Fasher

Katika kile kinachoonekana kuutetea mji huo kutodondokea mikononi mwa wanamgambo hao, jeshi la Sudan limeungana na makundi ya waasi na kuunda kikosi cha pamoja ili kuhifadhi udhibiti wa mji huo.

Wapiganaji wa kundi la RSFPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Mara kadhaa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa akilaani mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo wa RSF, ambayo yamesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makaazi yao huku wengine maelfu wakiuwawa.

Katika mkururo wa mashambulizi ya hivi karibuni Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric alizitaka pande zote "kujiepusha na mashambulizi yoyote ambayo yanaweza kuwadhuru raia au kuharibu miundombinu ya raia."

Soma pia:Mizozo iliopo kwenye mataifa ya Afrika imesahaulika?

Aidha Mkuu wa shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, nchini Sudan, Mohamed Refaat, amesema hali bado ni mbaya:

"Takriban watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao nchini Sudan, huku zaidi ya milioni mbili wakivuuka mipaka na kuingia katika nchi jirani,"

Alisema Refaat na kuongeza kuwa Wasudan wengi wamekuwa wakihasa Chad, Sudan Kusini na Misri,

"Mara nyingi wakifika katika mazingira hatarishi na wakikabiliwa na kiwewe cha hali ya juu." Alisema.

Vita kati ya RSF na jeshi la Sudan vimeharibu nchi hiyo vibaya huku mapigano yakienea katika miji mingi na kuwafanya wakazi wake kukabiliwa na njaa.

Zaidi ya watu 14,000 wameuawa na maelfu wamejeruhiwa, na wengine mamilioni wameyahama makazi yao.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

01:16

This browser does not support the video element.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW