Hukumu ya Uli Hoeness ni ya mwisho
17 Machi 2014Kumaanisha kuwa rais huyo wa zamani wa Bayern Munich anaweza sasa kuanza kutumikia kifungo hicho gerezani. Hoeness mwenye umri wa miaka 62, na ambaye ni mmoja wa watu maarufu zaidi katika soka la Ujerumani, alihukumiwa wiki iliyopita kwa kukwepa kulipa kodi ya kiasi cha euro milioni 28.5 kupitia yake ya benki ya Uswisi. Alisema kuwa hatokata rufaa na akajiuzulu kama rais wa Bayern. Hivyo basi anatarajiwa kuanza kutumikia kifungo chake katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Hoenness amepata mafanikio makubwa akiwa kama mchezaji na klabu hiyo ya mjini Munich , ambapo alijiunga na klabu hiyo mwaka 1970, akishinda vikombe vitatu vya ulaya. Lakini ni katika utendaji wake kama meneja mkuu ambapo aliibadilisha Bayern Munich kuwa moja kati ya vilabu vikubwa barani Ulaya.
Akikubali wadhifa mwaka 1979 akiwa na umri wa miaka 27 , muda wake wa kucheza kandanda ukiwa umemalizika mapema kutokana na kuwa majeruhi, Hoeness alitumia uwezo wake wa kibiashara na kampuni yake ya kutengeneza nyama za soseji barani Ulaya kuleta wafadhili na vitega uchumi katika muda wote wa uongozi wake wa miaka 31 katika klabu hiyo. Katika maelezo aliyoyatoa katika kituo cha televisheni cha taifa ARD mwenyekiti wa shirika linalopambana na rushwa duniani Transparency International nchini Ujerumani Caspar von Hauenschild amesema viatu vya Uli Hoenness ni ngumu kuvivaa wakati huu.
"Katika kila baraza la ushauri, mwenyekiti wa baraza hilo ndie mwenye mamlaka makuu, katika shirika lolote lile. Wakati inapotakiwa kuchukua maamuzi magumu sauti yake inakuwa nzito. Uzito wa sauti hii kwa Uli Hoeness kwa mtazamo wangu si rahisi kwa kweli kuipata tena."
Hoennes alikuwa rais wa Bayern Munich mwaka 2010, na mafanikio yaliendelea, kwa timu hiyo kushinda mataji matatu kwa msimu mmoja mwaka jana 2013. Kile anachokiacha Hoeness kwa klabu hiyo ni kwamba kuondoka kwa Hoennes itakuwa si rahisi lakini si kwanza haitawezekana kuiendeleza hali hiyo ya mafanikio. Bidhaa ambayo ni Bayern Munich itaendelea kuvutia soko duniani kote, wakati kikosi cha timu hiyo kina uwezo mkubwa hivi sasa katika Bundesliga ambapo fedha zinazopatikana kutoka katika kushiriki katika champions league hazitakatika. Herbert Hainer aliteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa baraza la ushauri la Bayern Munich, klabu hiyo imetangaza siku ya Ijumaa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef