1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoadhibiwa polisi wa Kenya ni hatari kwa Uchaguzi

2 Agosti 2022

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema leo kuwa, kitendo cha Kenya kutowawajibisha polisi kwa madai ya mauaji baada ya uchaguzi wa 2017, kunaongeza hatari ya uchaguzi ujao.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Tony Karumba/AFP

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema mamlaka nchini Kenya imeshindwa kuchunguza tuhuma za ukatili wa polisi au kufanya mageuzi, na kuwa hilo linaongeza tishio la ghasia iwapo matokeo ya uchaguzi wa wiki ijayo yatapingwa.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Afrika Mashariki, Otsieno Namwaya, amesema Kushindwa kukabiliana na unyanyasaji wa polisi katika uchaguzi uliopita wa Kenya, kuna hatari ya kuwasukuma kuendelea na mwenendo wao mbaya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Polisi wa Kenya mara nyingi wanashutumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kutekeleza mauaji kinyume cha sheria, hasa katika vitongoji maskini. Pia wamekuwa wakishutumiwa hapo awali kwa kuendesha vikundi vilivyowalenga wanaharakati na wanasheria wanaochunguza madai ya ukiukwaji wa haki unaofanywa na polisi.

Soma zaidi:Raila: Sishiriki mdahalo sababu Ruto ni fisadi 

Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Ripoti ya Human Rights Watch

Shirika la Human Rights Watch limesema limerekodi madai ya polisi kuendesha mauaji ya takriban watu 104 wakati wa uchaguzi uliopita wa mwaka 2017, wengi wao wakiwa wafuasi wa kiongozi wa upinzani wakati huo Raila Odinga. Maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami vikali walitumwa kuwatawanya waandamanaji baada ya Odinga kukataa kukubali ushindi wa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema, zikiwa zimesalia siku saba kabla ya uchaguzi mkuu mwingine, mamlaka za Kenya bado hazijachukua hatua kuhakikisha haki inatendeka kwa dhuluma za polisi ambazo zilijitokeza katika uchaguzi mkuu uliopita.

Picha: AP

Uchaguzi wa Kenya na matukio ya vurugu

Mnamo Agosti 9, Wakenya watamchagua rais mpya pamoja na mamia ya wabunge na takriban maafisa 1,500 wa kaunti. Kura ya urais mwaka huu kwa kiasi kikubwa itamchagua mshindi kati ya washindani wakuu wawili ambao ni Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga, ambaye sasa anaungwa mkono na Rais Kenyatta pamoja na chama tawala.

Kenya yenye idadi tofauti ya watu na makundi makubwa ya wapiga kura, imekuwa kwa muda mrefu ikikumbwa na ghasia za kijamii zinazochochewa na matukio ya kisiasa wakati wa uchaguzi. Uchaguzi wa mwaka 2007 ulipelekea zaidi ya watu 1,100 kupoteza maisha, na kusababisha jeraha la kitaifa.

Soma zaidi: Ghasia dhidi ya wanawake wanaowania viti vya siasa Kenya

Shirika la Human Rights Watch limebaini kuwahoji wanaharakati, maafisa wa serikali, maafisa wa polisi na familia za wahasiriwa ambao wanahofia kuwa vikosi vya usalama vitatumia nguvu kupita kiasi kwa ghasia zozote au maandamano ya umma yatakayoshuhudiwa ikiwa mizozo itazuka baada ya uchaguzi wiki ijayo.

Katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa Aprili 2022, muungano wa mashirika 15 ya kiraia ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch, ulirekodi matukio 219 kwa mwaka 2021 pekee, ikiwa ni pamoja na mauaji 187 yaliyofanywa na polisi huku watu 32 wakitoweka kusikojulikana.

 

Vyanzo: (AFP/HRW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW