1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights Watch na Amnesty: Hali ni mbaya mno Tanzania

28 Oktoba 2019

Ukandamizaji wa serikali ya Tanzania dhidi ya vyombo vya habari, watetezi wa haki za binadamu na vyama vya upinzani umeongezeka tangu mwaka 2015.Imesema ripoti ya mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International.

Präsident John Magufuli aus Tansania
Picha: Reuters/T. Mukoya

Ripoti zote mbili za mashirika hayo zimeeleza kuwa serikali ya Rais John Pombe Magufuli inatekeleza msururu wa sheria ambazo zinakandamiza uhuru wa wanahabari na kuzuia harakati za mashirika yasiyo ya kiserikali na upinzani wa kisiasa.

Mwezi ujao Rais John Magufuli atakuwa anaadhimisha miaka minne madarakani na afisa wa shirika la Human Rights Watch Audrey Wabwire anasema tangu aingie madarakani hali imekuwa si nzuri nchini humo katika masuala ya uhuru wa kujieleza.

Kituo cha Swahiba FM Zanzibar kilifungwa mwaka 2015

Tangu mwaka 2015 serikali nchini Tanzania imeongeza juhudi zake za kuvibana vyombo vya habari na imeyasimamisha kufanya kazi karibu magazeti matano kutokana na kile walichokichapisha kudaiwa kuwa taarifa zenye utata. Miongoni mwa magazeti hayo ni gazeti la The Citizen ambalo linachapisha taarifa zake kwa Kiingereza, lililofungiwa mwaka 2019 huku magazeti mengine manne yakifungiwa mwaka 2017.

Vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto TanzaniaPicha: DW/E. Boniphace

Kulingana na ripoti hiyo Tume ya Utangazaji ya Zanzibar ilikifunga kituo cha Redio cha Swahiba FM Oktoba 2015 kwasababu kiliripoti kuhusu kufutiliwa mbali na kufanyika kwa mara nyengine kwa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015.

Mashirika hayo ya Human Rights Watch na Amnesty yanasema kuwa utawala nchini Tanzania ulitumia kifungu cha sheria ya uhalifu wa mitandao cha mwaka 2015 kuwafungulia mashtaka waandishi wa habari na wanaharakati kutokana na taarifa walizoziweka kwenye mitandao ya kijamii. Mwaka 2017 Bob Chacha Wangwe ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu alifungwa kwasababu katika taarifa aliyokuwa ameiandika katika mtandao wa Facebook, aliitaja Zanzibar kama koloni la Tanzania bara.

Suala la kushambuliwa Tundu Lisu pia lipo katika ripoti hiyo

Ripoti hiyo pia inasema mwaka 2016 Rais Magufuli aliweka marufuku ya kutofanyika mikutano yote ya kisiasa hadi mwaka 2020 jambo linalokwenda kinyume na sheria za nchi hiyo. Marufuku hayo yamewekewa upinzani tu. Kutokea wakati huo wanasiasa kadhaa wa upinzani, wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa kukiuka amri hiyo ya rais.

Aliyekuwa mbunge wa upinzani Tundu Lissu alinusurika kifo baada ya kushambuliwaPicha: DW

Suala la kushambuliwa kwa mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu pia limetajwa katika ripoti hiyo.

Mashirika hayo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu sasa yanaitaka serikali ya Tanzani kuziheshimu haki za raia wake.

Mashirika hayo yanaitaka pia serikali ya Tanzania iwaachie huru waandishi wa habari na wanasiasa waliokamatwa na zaidi ya hayo iyafutilie mbali mashtaka yanayowakabili.