Human Rights Watch na hali nchini Burundi
19 Januari 2017Katika muda wa miezi mitatu iliyopita, wanachama wa kundi hilo la Imbonerakure kutoka kabila la Uhutu walitumia marungu kumpiga na kumuuwa kijana mmoja waumri wa miaka 15, kumdunga kijana mwengine kwa kisu jichoni na kumsababishia upofu na kuwashambulia wengine kwa marungu, visu na mbao.
Wanachama hao pia walimuuwa kijana mwengine kwa kumpiga kwa mawe na kuweka vizuizi vya barabarani kinyume cha sheria na wakati mwingine kuwazuia na kuwapiga wapita njia na kuwaibia fedha zao.
Raia nchini Burundi wanaishi kwa hofu ya mashambulizi zaidi na kuogopa kuyazungumzia ama kuyakosoa mauaji hayo, mateso na maovu mengine, anasema Ida Sawyer, mkurugenizi wa shirika hilo la kufuatilia haki za binadamu katika eneo la Afrika ya Kati.
Aliendelea kusema kuwa wauaji hao wanaotekeleza uovu huo bila kujali na maafisa wa serikali wanaowaunga mkono wanapaswa kufahamu kuwa kuna adhabu ya matukio hayo.
Vyombo vya habari nchini humo ambavyo awali vilikuwa vikakamavu na huru pamoja na mashirika yasiokuwa ya serikali yamekandamizwa na zaidi ya watu 325 elfu wameitoroka nchi hiyo.
Katika muda wa mwaka mmoja na nusu uliopita, mamia ya watu wameuawa na wengine kukabiliwa na mateso ama kutekwa nyara. Makundi ya upinzani yaliojihami pia yamewashambulia maafisa wa usalama na wanachama wa chama tawala ikiwa ni pamoja na polisi na wanachama wa Imbonerakure.Ripoti hii mpya ya shirika hilo linalofuatilia haki za binadamu yanatokana na mahojiano yaliofanywa tangu mwezi Oktoba mwaka 2016 na zaidi ya waathiriwa 20, wanaharakati wa kuteteta haki za binadamu na wengine ambao walitaja msururu wa maovu yaliotekelezwa na wanachama hao wa kundi la imbonerakure katika mikoa sita ya nchi hiyo.
Mawakili, mashahidi na mahakimu wanasema kuwa kesi zilizo na mwingilio wa kisiasa mara nyingi hushughulikiwa na mahakimu walio na ushirikiano wa karibu na chama tawala. Watu wengi hukataa kuwasilisha kesi dhidi ya kundi hilo la imbonerakure kwa kutokuwa na imani na mfumo wa mahakama wanaoamini hauwezi kuwasaidia na huenda unahusika katika maovu hayo.
Baraza la Umoja wa mataifa linalohusika na haki za binadamu liliidhinisha uamuzi mnamo mwezi September mwaka 2016 kuunda tume ya uchunguzi kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi tangu mwezi Aprili mwkaa 2015 na kubainisha iwapo ukiukaji huo unaweza kutajwa kama uhalifu wa kimataifa. Tume hiyo pia ina jukumu la kutambua wale waliohusika katika maovu hayo kwa lengo la kuhakikisha uwajibikaji. Maafisa wa serikali nchini Burundi wamekataa kushirikiana na tume hiyo.
Burundi ilitumbukia katika hali ya machafuko na uvunjaji sheria tangu mwaka 2015 wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza azma yake ya kuwania muhula wa tatu wa uongozi licha ya kuweko kwa mkataba ulioidhinishwa wa Arusha unaoruhusu kuhudumu kwa mihula miwili pekee.
Mwandishi: Tatu Karema/ HRW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman