HRW yaitaka Uganda kuchunguza ukatili wa polisi
28 Aprili 2020Human Rights Watch inaitaka serikali ya Uganda kuchunguza madai kuwa Francis Zaake aliteswa akiwa kizuizini,.
Kwa mujibu wa mtafiti katika shirika hilo la kutetea haki za kibinadamu nchini Uganda, Oryem Nyeko amesema "Ripoti kuwa Zaake aliteswa zinasikitisha. Mashahidi wametueleza kuwa walipomuona baada ya kukamatwa, hakuweza kutembea na alikuwa na majeraha. Ukatili wa polisi haukubaliki siku zote iwe nyakati za janga au la. Serikali ya Uganda inafaa kuhakikisha kuwa Zaake anapata huduma bora za matibabu na kuchunguza tukio hilo na kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua."
Haya yanajiri baada ya Rais Yoweri Museveni kuagiza polisi kuwakamata wanasiasa wanaosambaza chakula baada ya serikali kupiga marufuku usafiri wa umma, kusimamisha huduma zisizo muhimu na kufunga masoko ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.
Agizo hilo lilitolewa mnamo Machi, 30.
Rais Museveni aliagiza polisi kuwakamata wanasiasa wanaosambaza chakula
Serikali ilisema kuwa misaada yote ya chakula ilipaswa kupitia kwenye kamati maalum ya serikali kwa ajili ya usambazaji wa chakula.
Vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi wakati wa kutekeleza hatua zilizowekwa na serikali kudhibiti kasi ya maambukizo ya virusi vya Corona. Human Rights Watch imesema vikosi hivyo vimekuwa vikiwapiga watu risasi, vikiwakamata watu kiholela wakiwemo wachuuzi, na watu wenye kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Vile vile, kamati ya kulinda waandishi wa habari imeripoti kuwa vikosi vya usalama nchini humo vimewashambulia na kuwanyanyasa takribani wanahabari 6 tangu tarehe 19 mwezi Machi.
Polisi ilimkamata Zaake nyumbani kwake Mityana, takribani kilomita 70 kaskazini mwa Kampala alipokuwa akigawa chakula kwa watu walioathirika na vizuizi vya serikali katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.
Zaake alizuiliwa katika kitengo cha upelelezi kilichoko Kireka, Kampala, na awali polisi iliinyima familia yake na hata wakili wake fursa ya kumuona.
Hata hivyo, polisi imekanusha ripoti kuwa Zaake aliteswa. Lakini mashahidi watatu waliiambia Human Rights Watch kuwa Zaake hakuweza kutembea vizuri kutokana na kipigo.
Mbunge wa Jinja Paul Mwiru pamoja na wakili Meddard Sseggona waliomtembelea Zaake akiwa hospitali wanasema kuwa alikuwa na majeraha mabaya.
Polisi ya Uganda imekuwa na rekodi ya kunyanyasa wapinzani. Mnamo mwaka 2018, wanajeshi waliwashambulia Zaake akiwa na wenzake 32 akiwemo mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi maarafu kama Bobi Wine katika eneo la Arua.