HRW yasema waasi wa M23 huenda walihusika na mauaji Kishishe
14 Juni 2023Miili hiyo inaaminika kuwa ni ya wanavijiji na wanamgambo waliotekwa na baadae kuuliwa na waasi wa M23, kati ya Novemba 2022 na Aprili 2023, wakati kundi hilo lilipokuwa likiondoka Kishishe.
Human Rights Watch imerekodi visa vya mateso vilivyofanywa na waasi wa M23 katika eneo hilo la Kishishe baada ya kuzungumza na mashuhuda, kutizama picha za satelaiti, za kawaida na za video.
Soma zaidi: Waasi wa M23 wahusishwa na makaburi ya pamoja nchini DRC
Pamoja na visa hivyo vya mateso, waasi hao wa M23 walichoma moto nyumba moja iliyokuwa imefurika miili, kutumia shule tatu kama kambi zao, ingawa baadae walichoma moja ya shule hizo, hatua iliyowanyima watoto fursa ya kusoma.
Wakazi wa Kishishe walishuhudia mauaji ama mazishi ya miili hiyo wamesema kwamba makaburi ya pamoja yaliyorundikwa miili karibu 20 kwa kila kaburi yalichimbwa baada ya M23 kulidhibiti eneo hilo na baada ya kuondoka, baadhi ya makaburi ndipo yalipogunduliwa.