Human Rights Watch: Watu 700 wameuawa Kongo
7 Oktoba 2016Shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch limesema wapiganaji wasiofahamika wamewaua karibu raia 700 katika mfululizo wa mashambulizi yaliyoanza miaka miwili iliyopita wilaya ya Beni mashariki mwa jamuhuri ya Kidemocrasi ya Kongo. Mauji hayo yameendelea licha ya kuwepo majeshi ya Kongo na walinda amani wa Umoja wa mataifa.
Shambulizi kubwa na la karibuni lilifanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo wapiganaji waliua karibu watu 40 na kuteketeza nyumba kadha katika mji wa Rwangoma uliojirani ya mji wa beni. Serikali ya Kongo na walinda amani wa umoja wa mataifa wametakiwa kuibuka na mikakati mipya ya kuwalinda wananchi hasa walioko mji wa Beni na kuhakikisha wanaohusika na mashambulizi hayo wanachukuliwa hatua.
Baada ya miaka miwili ya mauji ya kikatili,wenyeji wa Beni wanaishi kwa hofu ya kutokea mashambulizi zaidi na hata wamepoteza matuamini kuwa kuna yeyote anaweza kuyamaliza mauji yanayoendelea. Watafiti wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, wanasema ripoti za kuaminika kutoka wanaharakati wa Kongo na pia kutoka shirika la Umoja wa mataifa zinaonyesha kuwa wapiganaji wenye silaha wamewaua karibu raia 680 katika angalau mashambulizi 120 wilaya ya Beni tangu mwezi October mwaka 2014.
Waathirika na mashahidi walieleza jinsi washambuliaji hao walivyofanya mauji hayo kwa kuwakatakata kwa shoka au mapanga hadi kufa wahusika huku wengine wakipigwa risasi. Idadi ya wahanga huenda ikiwa juu kuliko ilivyo sasa
Kufikia sasa haieleweki wanaofanya mashambulizi hayo. Serikali ya Kongo inalilaumu kundi moja la waasi ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake katika eneo hilo, huku vyanzo vingine vikiyahusisha makundi mengine na hata maafisa wa kijeshi na baadhi ya mashambulizi.
Mauaji yaendelea licha ya kuwepo wanajeshi
Ripoti hiyo ya Human Rights Watch inatokana na tafiti tano zilizofanywa wilaya ya Beni tangu mwezi Novemba mwaka 2014, mahojiano ya zaidi ya waathirika 160 na mashahidi waliyoyashuhudia mashambulizi hayo. Wengine waliohojiwa ni maafisa wa jeshi la kongo,Umoja wa mataifa,wale wa serikali ya Kongo miongoni mwa wengine. Wakati wa Mahojiano hayo mvulana mwenye umri wa miaka 10 alieleza jinsi alivyochukuliwa mateka wakati wa shambulizi la mji wa Rwangoma na alishuhudia mauji kadhaa. Wanajeshi wa Kongo na wale wa Umoja wa mataifa walipelekwa eneo hilo baada ya kumalizika mashambulizi na wauji wakiwa tayari wametoroka zamani.
Mwandishi:Jane Nyingi/Human Rights Watch Report
Mhariri:Yusuf Saumu