1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights Watch yataka upelelezi ufanyike

29 Agosti 2012

Kufuatia kuuawa kwa mhubiri Aboud Rogo mjini Mombasa, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch sasa limeitaka serikali ya Kenya ifanye uchunguzi juu ya mauaji hayo na ghasia zilizozuka.

Polisi wa Mombasa, Kenya
Polisi wa Mombasa, KenyaPicha: dapd

Aboud Rogo, aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya kumiliki silaha kimagendo na kutafuta watu wa kujiunga na kundi la waislamu wenye itikadi kali la al-Shabaab, aliuliwa siku ya Jumatatu kwa kupigwa risasi alipokuwa akiendesha gari lake nje ya mji wa Mombasa. Kufuatia mazishi yake yaliyofanyika siku hiyo ya Jumatatu, machafuko yalizuka katikati ya mji wa Mombasa na kuendelea hadi leo. Magari yalichomwa moto, makanisa yalivamiwa na watu wasiopungua wawili waliuwawa. Mmoja wao alikuwa afisa wa magereza aliyekuwa akishirikiana na polisi kutuliza ghasia na wa pili alikuwa raia wa kawaida aliyeuwawa na waandamanaji. Polisi wa mjini Mombasa waliwaambia waandishi wa habari kwamba wamewakamata watu 23 wanaotuhumiwa kuhusika na machafuko yaliyotokea.

Akizungumza na DW kwa njia ya simu, Ben Rawlence wa shirika la Human Rights Watch ambaye kwa sasa yuko Mombasa, Kenya, alisema kwamba Rogo aliwaeleza polisi kwamba alikuwa akihofia usalama wake. "Aliomba kulindwa na serikali," alisema Rawlence. "Hata kama mtu yuko katika orodha ya magaidi bado kuna sheria inayotakiwa ifuatwe na ilipaswa Rogo aende mahakamani na si kuuliwa mtaani."

Aboud Rogo alipokuwa katika mahakama kuu jijini NairobiPicha: dapd

Naye Leslie Lefkow, ambaye ni naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika, amewataka polisi wa nchini Kenya wazingatie sheria katika kudhibiti ghasia zilizotokea baada ya kifo cha Rogo.

Washukiwa wengine wametekwa au kuuawa

Kifo hicho kimekuja baada ya visa vingine vya utekaji nyara na hata mauaji ya watu walioshukiwa kutafuta wapiganaji wa kujiunga na kundi la al-Shabaab na kufanya makosa mengine yanayohusishwa na kundi hilo.

Mwezi Machi mwaka huu, Samir Khan, ambaye pia ameshtakiwa kwa makosa hayo, pamoja na rafiki yake Mohammed Kassim, walitolewa kwa nguvu kutoka katika basi moja mjini Mombasa. Wakili wa Khan, Bw. Mbugua Mureithi, ameeleza kwamba waliolisimamisha basi hilo ni watu waliojitambulisha kuwa polisi. Siku chache baadaye, maiti ya Khan iliyokuwa imeharibiwa vibaya, ilikutwa katika mbunga ya wanyama ya Tsavo.

Gari alilokuwa akiendesha Rogo aliposhambuliwa na risasiPicha: Reuters

Mpaka sasa haifahamiki Mohammed Kassim alipo. Kabla ya kutolewa katika basi, mwezi Februari mwaka huu, Kassim alitekwa nyara na kuachiwa baada ya kuhojiwa na wale waliomteka. Polisi walifanya mkutano na waandishi wa habari na kuarifu kwamba Kassim alikuwa ametekwa na polisi wa kupambana na ugaidi. Hata hivyo, polisi hao baadaye walikanusha kuhusika na utekaji nyara uliofanyika.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/HWR

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW