1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huyu ndiye mkuu mpya wa NATO

1 Oktoba 2024

Muungano wa Kijeshi wa NATO umepata kiongozi mpya, Mark Rutte, aliyekuwa waziri mkuu wa Uholanzi, anayechukuwa nafasi ya Jens Stoltenberg. >Je, Rutte ni nani na anakabiliwa na changamoto gani?

Katibu Mkuu mpya wa NATO, Mark Rutte.
Katibu Mkuu mpya wa NATO, Mark Rutte.Picha: Gene Medi/NurNurPhoto/picture alliance

Julai 2023,  Rutte alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu wa Uholanzi na miezi michache baadaye akaanza kudhihirisha nia yake ya kumrithi Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ambaye alitangaza kuachia wadhifa huo ifikapo Septemba 2024.

Kwa miezi kadhaa, Rutte aliendesha kampeni yake ndani ya muungano wa NATO, huku viongozi wengi wakiwa tayari wanamfahamu alipokuwa waziri mkuu wa Uholanzi kwa zaidi ya miaka 13 ya kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya kimataifa. 

Soma zaidi: Mfahamu Katibu Mkuu Mpya wa NATO

Mwanahistoria huyo, ambaye ni mgombea aliyepigiwa pia upatu na Rais Joe Biden wa Marekani na viongozi wengi wa Ulaya, anakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na vita nchini Ukraine, hofu juu ya hatua za baadaye za Urusi na hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Marekani kutokana na kutofahamu kwa sasa ni nani atayeshinda urais.

Wakati wa hotuba ya kuaga, Stoltenberg aliyaelezea hayo kuwa ni sehemu ya changamoto zinazoikabili NATO.

Katibu Mkuu wa NATO aliyemaliza muda wake, Jens Stoltenberg (kulia).Picha: Jakub Porzycki/NurPhoto/picture alliance

"Tangu nichukue wadhifa wangu kama katibu mkuu mwaka 2014, ulimwengu unaotuzunguuka umebadilika sana. Tumeshuhudia Urusi ikiinyakua kinyume cha sheria rasi ya Crimea, kuimarika kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS), uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, ushindani unaokua wa China, janga la UVIKO-19, mashambulizi zaidi ya mtandaoni na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye usalama wetu."

Changamoto ya mpasuko ndani ya NATO

Mbali na hayo, Rutte anakabiliwa pia na changamoto ya kuyaleta pamoja maono ya viongozi wa nchi wanachama ili hatimaye kuwepo makubaliano ya pamoja linapokuja suala la maamuzi muhimu.

Rutte ni mzoefu katika kuongoza miungano ya kisiasa nchini Uholanzi, lakini sasa atatakiwa kuvileta pamoja vyama 32 ili kufikia mwafaka unaohitajika kwa maamuzi yote ya NATO.

Soma zaidi: Rutte kuanza uongozi wa NATO

Katika kampeni yake, Rutte alikuwa na kibarua kigumu cha kumkinaisha Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambaye hapo nyuma mahusiano yao yalikuwa na mkwaruzano. 

Viongozi wa NATO wakiwa kwenye mkutano wa Brussel.Picha: EPA/OLIVIER HOSLET

Rutte alilazimika kumuahidi Orban kwamba Hungary haitalazimika kamwe kushiriki katika shughuli za kusaidia Ukraine nje ya eneo la NATO.

Orban, ambaye anadumisha uhusiano wa kirafiki na Urusi, amekataa pia kupeleka silaha kwa Ukraine. 

Siasa za kiliberali za Rutte na msimamo wa siasa kali za mrengo wa kulia za Orban mara nyingi huwaweka kwenye mzozo katika shughuli zao ndani ya Umoja wa Ulaya.

Hungary ilipopitisha sheria dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ+) mwaka wa 2021, Rutte alimwambia Orban kuwa yuko huru kuondoka katika jumuiya hiyo iwapo hakubaliani na sera zake.

Haiba ya Rutte na misimamo yake

Uwezo wake mashuhuri wa kukabiliana na changamoto za kisiasa na kuwa na misimamo isioyumba, unamfanya Rutte kuwa kiongozi anayefaa iwapo Donald Trump atarejea katika Ikulu ya White House na kuanza ukosoaji wake dhidi ya muungano huo wa kijeshi. 

Mabadiliko ya uongozi kwenye Jumuiya ya kijeshi ya NATO

This browser does not support the audio element.

Hata hivyo, cha kushangaza Rutte na Trump walikuwa na uhusiano mzuri wakati wa muhula wa kwanza wa Trump kama rais wa Marekani, na Trump alifikia hata kumwita Rutte "rafiki", lakini Rutte alipinga vikali sera ya uchumi ya Trump.

Tofauti na Trump, Rutte ni muungwaji mkono mkubwa wa Ukraine na aliwezesha uwasilishaji wa silaha mjini Kyiv, ikiwa ni pamoja na vifaru na ndege za kivita chapa F-16.

Wachambuzi wanasema Rutte atatakiwa kuonyesha dira ya uongozi wake ili kuiendeleza NATO, kwa sababu kufikia muafaka kunaweza kuchukua muda na inaweza kukatisha tamaa lakini ni muhimu kuonyesha mwelekeo wa kisiasa na maendeleo yanayofikiwa