IAEA: Iran inaongeza akiba yake ya madini ya urani
18 Novemba 2021Shirika hilo la IAEA limeziambia nchi wanachama katika ripoti yake ya siri ya kila robo mwaka iliyotolewa Jumatano kwamba Iran ina wastani wa akiba ya kilo 17.7 za madini ya urani iliyorutubishwa katika kiwango cha hadi asilimia 60, ongezeko la karibu kilo 8 tangu mwezi Agosti na kukiuka mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 uliosainiwa kati ya Iran na nchi zenye nguvu duniani.
IAEA imesema kiasi hicho cha madini ya urani yaliyorutubishwa kinaweza kutumika kwa urahisi kutengeza silaha za atomiki, jambo ambalo mataifa yenye nguvu duniani yanajaribu kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran.
Akiba kamili haijathibitishwa
Shirika la IAEA lenye makao yake mjini Vienna, Austria limesema kwamba bado halijaweza kuthibitisha akiba kamili ya madini ya urani iliyorutubishwa ya Iran, kutokana na vizuizi ambavyo Iran imeviweka dhidi ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika ripoti tofauti kwa nchi wanachama kuhusu kazi ya shirika hilo nchini Iran, mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi amesema wana wasiwasi kuhusu wakaguzi kukaguliwa kupita kiasi na maafisa wa usalama katika vinu vya nyuklia nchini Iran.
''Mwezi Septemba, IAEA ilifikia makubaliano na Iran kwamba wakaguzi wa shirika wataendelea na shughuli za shirika hilo kusimamia na kukagua vifaa. Hata hivyo, shirika halijafanikiwa kukifikia hata kinu kimoja, jambo ambalo linamaanisha kwamba shirika linaamini kuwa shughuli za kudumisha mwendelezo wa maarifa muhimu ya JCPOA zinapungua,'' alifafanua Grossi.
Grossi amerudia wito wake kwa Iran kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo na kutekeleza taratibu za usalama katika vinu vya nyuklia ambazo zinaendana na taratibu za usalama za kimataifa na wajibu wa kisheria wa Iran kuhusu haki na kinga za shirika hilo na wakaguzi wake.
Mkuu wa IAEA kuizuru Iran
Wakati huo huo, Grossi anatarajiwa kuizuru Iran Jumatatu ijayo kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana na maafisa wa Iran kuhusu juhudi za kuliwezesha Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, kufahamu kile kinachoendelea nchini humo kuhusu mpango wa nyuklia.
Ama kwa upande mwingine, ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE unatarajiwa kuizuru Iran hivi karibuni, wakati ambapo taifa hilo la Ghuba linafanya kazi ya kutuliza mivutano na Iran. Afisa wa UAE amesema mshauri wa masuala ya usalama wa kitaifa, Sheikh Tahnoon bin Zayed Al Nahyan atauongoza ujumbe huo. Sheikh Tahnoon ni kaka wa kiongozi wa Abu Dhabi, Mwana Mfalme Mohammed bin Zayed na mwenyekiti wa shirika la uwekezaji la serikali ADQ.
(AP, AFP, Reuters)