1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA: Iran yapanua uwezo wa kurutubisha madini ya urani

2 Desemba 2021

Wataalamu wa shirika la IAEA wamesema Iran inapanua uwezo wake wa kurutubisha madini ya urani na kukiuka masharti ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.

Tschechien AKW Dukovany
Picha: Zoonar.com/www.artushfoto.eu/picture alliance

Katiku ujumbe kwa mataifa wanachama wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, IAEA imesema kuwa siku ya jumanne, wakaguzi wake walitembelea kinu cha nyuklia cha chini ya ardhi cha Fordow na kuripoti kwamba hatua zimechukuliwa katika kinu hicho kurutubisha madini ya Urani kwa kutumia mitambo ya kisasa.

Tangazo hilo lilionekana kudhoofisha mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ya kutaka kuyarudisha kikamilifu mataifa yote mawili katika mkataba wa nyuklia ulioparaganyika yaliyoanza tena wiki hii baada ya mapumziko ya miezi mitano kutokana na kuchaguliwa kwa Rais Ebrahim Raisi wa Iran aliye msimamo mkali.

Wapatanishi wa nchi za Magharibi wanahofia kuwa Iran inatafuta ukweli kuhusu suala hilo ili kuwa na nguvu katika mazungumzo hayo. Iran imethibitisha kuwa mchakato wa kurutibisha asilimia 20 ya  urani yake umeanza katika kinu hicho cha Fordow. Katika kujibu ripoti hiyo, mkuu wa ujumbe Iran mjini Vienna, Mohammed -Resa Ghalebi, amesema kuwa urani hiyo ni ya kutengeneza kemikali ya hexafluoride ambayo matumizi yake ni ya amani. Hata hivyo Ghalebi amesema kuwa wakaguzi hao wa IAEA waliruhusiwa kuingia katika kinu hicho kufanya ukaguzi wao. Haya yameripotiwa na shirika la Habari la ISNA.

Rafael Mariano Grossi - Mkurugenzi mkuu IAEAPicha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Shirika la habari la reuters limeripoti kuwa ripoti ya kina ya shirika hilo la IAEA iliyosambazwa kwa mataifa wanachama wake inasema kuwa kutokana na hatua ya Iran, shirika hilo linapanga kuongeza ukaguzi katika kinu hicho cha Fordow  kinachohifadhi mitambo ya kisasa ya urutubishaji lakini bado hakuna maelezo zaidi.

Iran imepuuza ripoti hiyo kuwa ya kawaida licha ya ukweli kwamba shirika la IAEA, ambalo halitoi sababu kwa uwazi kuhusu ripoti hizo , kwa kawaida huzitoa kwa ajili ya matukio muhimu pekee kama vile ukiukaji mpya wa vikwazo vya nyuklia vya mkataba.

Yaliokuwemo katika mkataba wa nyuklia wa 2015

Mkataba wa kihistoria wa 2015 uliweka vikwazo kwa mpango wa nyuklia wa Iran kuizuia kutengeneza silaha za nyuklia na kutokana na hilo, nchi za Magharibi ziiiondolee Iran vikwazo. Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China zilisimamia mazungumzo hayo. Wanadiplomasia wa ulaya walikuwa na matumaini ya ishara ya nia njema kutoka Iran. Hata hivyo, Iran  ilianza kukiuka taratibu za makubaliano na kusababisha Marekani kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia mnamo 2018 chini ya rais Donald Trump na kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW