Ibada kuwakumbuka wahanga wa mashambulio ya wanazi mambo leo
23 Februari 2012Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanachambua kwa hivyo umuhimu wa siku ya leo kwa jamii ndani na nje ya Ujerumani .
Tuanze na gazeti la "Berliner Morgenpost" linaloandika"Maandalizi ya leo ya kuwakumbuka wahanga wa matumizi ya nguvu ya wafuasi wa siasa kali ya mrengo wa kulia yanatoa fursa kwa watu kutafakari kwa dhati.Si suala la msiba uliotokea mwongo uliopita,ni suala linalohusiana na mauwaji yaliyochochewa na chuki ,yaliyotokea kati kati ya jamii hivi karibuni.Mauwaji ambayo hakuna hata mmoja aliyefikiria kama yangeweza kutokea.Hakuna wakati wowote,na nadra tangu utawala wa wanazi ulipotoweka,kuona msiba kama huu ukijadiliwa kama wakati huu ambapo watu wanajiuliza pia kuhusu jukumu la kila mmoja wetu.Hakuna anaeweza kuwanyooshea kidole cha shahada kundi dogo la wasiokuwa na haya.Hasa,mauwaji yaliyofanywa na kundi la makatili la Zwickau limetubainishia sote tena kwa machungu,kwa jinsi gani tunajikuta tukishawishika kwa dhana na kutupiana lawama.
Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linahisi kumbu kumbu hizi ni hatua ya mwanzo tuu na kuendelea kuandika:"Kuwakumbuka wahanga ni hatua ya kwanza tu.Ni hatua muhimu kwasababu inatoa ishara kwa ulimwengu mzima kwamba hisia za chuki dhidi ya wageni hazipuuzwi nchini Ujerumani au watu kuzimezeya.Hata hivyo kumbu kumbu hizo zinabidi zifuatiwe na fikra, mawazo na watu kutafakari.Kila mmoja wetu anabidi ajiulize anaweza kuchangia kwa jinsia gani ili hisia za chuki dhidi ya wageni na siasa kali ya mrengo wa kulia zisiwe na nafasi humu nchini?Si suala la kuona kuna siku moja iliyowekwa katika kalenda kuwakumbuka wahanga.Na wala si suala la kuonyesha picha ya hisia za chuki dhidi ya wageni na kwa namna hiyo picha mbaya kuhusu Ujerumani.Hasha.Ni suala linalohusu jinsi ya kukabiliana kwa dhati na kitisho cha makundi ya siasa ya mrengo wa kulia.
Gazeti la "Märkische Allgemeine" linandika:"Ibada rasmi inayofanyika katika jengo la burudani mjini Berlin na watu kusalia dakika moja kimya kote nchini Ujerumani ni juhudi za jamii ya kidemokrasi kutaka kuuonyesha ulimwengu na pia baadhi ya wananchi wenye mtazamo wa aina nyengine,kwamba shirikisho la jamhuri ya Ujerumani si mahala pa chuki dhidi ya wageni.Wote wale,na ambao pengine ndio wengi,waliokuwa wakiamini kwamba siasa kali ya mrengo wa kulia si kitisho hivyo kwa Ujerumani wamejifunza kutokana na visa vya mauwaji yaliyofanyawa na kundi la wananzi mambo leo wa Zwickau.Ni muhimu kwetu sisi na kwa maadili yetu kuhakikisha kwamba kumbu kumbu hizi zinaangaliwa kama njia ya kutafakari.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman