1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSaudi Arabia

Ibada ya Hijjah yaanza leo Ijumaa huko Makkah

14 Juni 2024

Mamilioni ya Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani wamekusanyika katika mji wa Makkah kushiriki ibada muhimu ya Hijjah inayoanza leo Ijumaa (14.06.2024).

Saudi Arabia - Ibada ya Hijjah 2024
Waumini wa kiislamu wakiwa wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makkah wakiizunguuka al-KaabaPicha: Abdel Ghani Bashir/AFP/Getty Images

Ibada hiyo ambayo ni moja kati ya nguzo tano za kiislamu inafanyika mwaka huu katika hali ya joto kali pamoja na vita vinavyowakabili Wapalestina. Waumini wa kiislamu wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makkah ambako wataanza kwa kuizunguuka al-Kaaba na kisha wataelekea huko Minnah ambako watalala kwenye mahema. Mamlaka nchini Saudi Arabia inakadiria kuwa mahujaji karibu milioni mbili ndiyo watakaoshiriki ibaya ya Hijjah mwaka huu.

Siku ya pili inayochukuliwa kama kilele cha ibada hii ya  Hijjah, mahujaji wataelekea kwenye Mlima wa Arafat, uliopo karibu kilomita 20 mashariki mwa mji wa Makkah, ambako hukaa huko na kufanya ibada hadi jua linapozama. Kwa waislamu ambao hawakushiriki Hijjah katika siku hiyo ya Arafat, wanashauriwa kufanya ibada ya funga yenye ujira mkubwa wa kufutiwa madhambi yao ya mwaka uliotangulia na ujao.

Ili kushiriki ibada hijjah ambayo hufanyika kuanzia siku ya nane hadi ya 12 ya Dhu al-Hijjah, ambao ni mwezi wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu, wanaume huvaa nguo nyeupe zisizo na mshono huku wanawake wakishauriwa kuvaa nguo zenye stara na wote kwa pamoja huambatana katika kila hatua ya Hijjah ili kuonyesha umoja, usawa na muamko wa kiroho, mambo yanayozingatiwa mno na dini ya Kiislamu.

Ibada ya Hijjah yagubikwa na joto kali na vita vya Gaza

Hali ya joto katika mji wa Makkah na vitongoji vyake inatarajiwa kufikia hadi nyuzijoto 43 katika viwango vya Celsius.Picha: Rafiq Maqbool/AP Photo/picture alliance

Hali ya joto katika mji wa Makkah na vitongoji vyake inatarajiwa kufikia hadi nyuzijoto 43 katika viwango vya Celsius, na mamlaka ya Saudia imewataka mahujaji kubeba miavuli na kuchukua hatua nyingine ili kujilinda wenyewe na jua kali wakati wa ibada.

Hijjah ya mwaka huu  inafanyika katika hali ya masikitiko kwa jamii ya waislamu kutokana na vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanaharakati wa Kipalestina wa Hamas.

Mwaka huu Wapalestina huko Gaza hawakuweza kusafiri hadi Makkah kushiriki ibada ya Hijjah kutokana na kufungwa mwezi uliopita kwa kivuko cha Rafah kinachopakana na Misri. Amna Abu Mutlaq, 75, amekosa pia fursa ya kuhiji kutokana na vita:

" Tumezuiliwa kufanya Hijjah kwa sababu ya kufungwa kwa mpaka kutokana na na vita, na hivyo hatuwezi kuondoka, na kila tunapojaribu kuondoka, tunaambiwa kuwa kivuko kimefungwa, na hivyo hatuwezi kuondoka. Wanatunyima haki ya kila kitu."

Hijjah, mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, ni wajibu kwa muislamu yeyote kuitekeleza ibada hii japo mara moja katika maisha yake ikiwa hali ya kifedha na kiafya itamruhusu.

Kufanya hivyo na kupata pia fursa ya kuutembelea mji wa Makkah alikozaliwa Kiongozi wa Waislamu Mtume Muhammad (SAW).

(Vyanzo: DPAE/APE)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW