Ibada ya kitaifa ya kumuaga Odinga yafanyika Nairobi
17 Oktoba 2025
Wakati jeneza la hayati Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga lilipowasili kwenye uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, mayowe, vilio, na firimbi zilisikika kutoka kwa umati muliokuwepo uwanjani hapo. Vikosi vya taifa viliungana na kwa pamoja kuchukua usukani ili kumpa marehemu Raila Odinga heshima kamili za kiongozi wa taifa.
Viongozi wa mataifa mbalimbali walipata fursa kutoa heshima zao za mwisho akiwemo rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, mabalozi na wageni rasmi.
Usalama watawala kwenye shughuli ya ibada
Mapema asubuhi, wabunge, mawaziri na viongozi serikalini walipata fursa kumuaga rasmi hayati naibu waziri mkuu wa zamani Raila Odinga kwenye majengo ya bunge. Umati ulitulia pindi wanawe walipopanda jukwaani kuzungumza na bintiye hayati Rosemary Odinga aliwashukuru waombolezaji kwa kumuenzi kigogo huyo.
Shughuli hiyo ilitibuka siku ya Alhamisi kwani umati wa waombolezaji uliojitokeza uliwazidi nguvu maafisa wa usalama. Siku ya Ijumaa, usalama uliimarishwa katikati ya jiji la Nairobi na ugani Nyayo kwenyewe.
Mjane Mama Idah Odinga aliwarai wakenya kusameheana na kuimarisha uhusiano katika jamii. Maziko rasmi yamepangwa kufanywa siku ya Jumapili nyumbani kwake Bondo kaunti ya Siaya.