Ibada ya kumuaga Jimmy Carter kufanyika Washington Januari 9
31 Desemba 2024Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye mwaka jana alisema Carter alimuomba atoe hotuba ya hadithi ya maisha kwenye mazishi yake, ameagiza kwamba Januari 9 iwe siku ya kitaifa ya maombolezo ya Carter kote Marekani. Siku sita za mazishi rasmi ya kitaifa ya Carter zitaanza Jumamosi.
Jeshi limesema mwili wake utasafirishwa kwa msafara wa magari kupitia mji aliozaliwa wa Plains, jimboni Georgia. Msafara huo utasimama shambani alikokulia. Kisha mwili wa Carter utasafirishwa hadi Atlanta, ambako utalala katika Kituo cha Carter hadi asubuhi ya Januari 7.
Kisha baadae mwili utasafirishwa hadi Washington, DC ambako utalazwa katika majengo ya Bunge la Marekani - Capitol Hill hadi pale itakapofanyika ibada ya kitaifa ya kuuaga. Atazikwa Georgia Januari 9 pembeni ya mke wake, Rosalynn Carter, nyumbani kwao mjini Plains.