1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini iliipuza wajibu wa kumkamata Omar al-Bashir

Sylvia Mwehozi
6 Julai 2017

Majaji wa mahakama ya ICC wamesema katika hukumu yao alhamis ( 06.07.2017) kuwa Afrika Kusini ilipuuza wajibu wake mwaka 2015, kwa kushindwa kumkamata rais wa Sudan Omar al-Bashir anayetakiwa na mahakama hiyo.

Südafrikas Präsident Jacob Zuma besucht Süd-Sudan Omar Al-Bashir
Picha: picture alliance/dpa/N.Mokoena

Hukumu hiyo iliyotarajiwa imeikuta na hatia Afrika Kusini kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake na kuzuia kazi ya mahakama pekee ya kudumu ya uhalifu wa kivita, ambayo pia ni nchi mojawapo mwanzilishi wa mahakama hiyo.

"Mahakama inahitimisha kwamba kwa kutomkamata Omar al-Bashir wakati akiwa katika eneo lake, Afrika Kusini ilishindwa kutekeleza ombi la mahakama la kukamatwa na kumsalimisha kiongozi wa Sudan", alisema jaji kiongozi Cuno Tarfusser.

Ameendelea kusema, hiyo ilikuwa ni kinyume na mkataba unaoongoza mahakama hiyo wa Roma na iliizuwia ICC kumshitaki Bashir kwa makosa 10 ya uhalifu wa kivita, yakiwemo matatu ya mauaji ya kimbari katika mkoa huo wa Magharibi mwa Sudan wa Darfur.

Lakini majaji hao wameshindwa kulipeleka suala hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa hatua zaidi, huku jaji Tarfusser akisema "rufaa haitakuwa na matokeo yoyote."

Wananchi wakimpokea rais Omar al-Bashir aliporudi kutoka Afrika Kusini 2015Picha: picture-alliance/dpa/M. Ali

Licha ya waranti mbili za kimataifa zilizotolewa 2009 na 2010, Bashir kwa kiasi kikubwa amesalia ofisini wakati migogoro ikiendelea kutokea katika mkoa huo wa Darfur.

Mwaka 2015, alihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika jijini Johannesburg licha ya hapo awali kuwepo na majadiliano na ICC na maafisa wa Afrika Kusini, baadae  aliondoka nchini humo bila ya kuzuiliwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiomba mahakama hiyo mwaka 2005 kuchunguza uhalifu uliofanywa Darfur ambako karibu watu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.5 kukosa makazi tangu makabila madogo yalipochukua silaha dhidi ya serikali ya kiarabu ya Bashir mwaka 2003, kwa mujibu wa tawkimu za Umoja wa Mataifa.

Mawakili wa Pretoria  walitoa hoja mwezi Aprili katika mahakama hiyo kuwa "hapakuwa na jukumu chini ya sheria za kimataifa kwa Afrika Kusini kumkamata Bashir" na kudai kwamba "hapakuwa na chochote" katika azimio la Umoja wa Mataifa la kuondoa kinga yake ya kidiplomasia.

Lakini mwendesha mashitaka wa ICC Julian Nicholls alitoa hoja kwamba Afrika Kusini "ilikuwa na uwezo wa kumkamata na kumsalimisha lakini ilichagua kutofanya hivyo."

Rais Omar al-Bashir akiwa na rais wa Rwanda Paul Kagame mjini KigaliPicha: picture-alliance/dpa/P.Siwei

Hatimaye, sababu pekee ya kwanini Afrika Kusini "haikumkamata ni kwamba, haikubaliani na sheria zilizowekwa, kwahiyo haikutii," alisema Nicholls.

Majaji walikubaliana katika hukumu ya alhamis kwamba majukumu ya kimataifa hayawezi kuwekwa kando kirahisi kama nchi haikubaliani nazo na kuamua kwamba katika kesi hii Bashir hakuwa na kinga.

Bashir ambaye amekuwa rais wa Sudan tangu mwaka 1993 amekana mashitaka yote na ameendelea kusafiri huku Khartoum ikitangaza jumatatu wiki huu kuwa ataitembelea Moscow kwa mara ya kwanza mwezi Agosti . Urusi ilitangaza mwishoni mwa mwaka jana kuwa inaondoa saini yake katika sheria ya Rome.

Mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague haina polisi na imekuwa ikitegemea nchi nyingine kuwakamata watuhumiwa au kuwasalimisha washukiwa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW