1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKimataifa

ICC na wafanyakazi wake walengwa na visa vya ujasusi

4 Juni 2024

Taarifa za vyombo vya habari zinasema Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC na wafanyakazi wake wanakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka nje. Mahakama hiyo ya mjini The Hague, Uholanzi imekuwa ikilengwa na visa vya ujasusi.

The Hague, Uholanzi | Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague, UholanziPicha: Klaus Rainer Krieger/reportandum/IMAGO

Ripoti ya gazeti la The Guardian nchini Uingereza imefichua madai kwamba mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Israel Yossi Cohen, alimuwekea shinikizo mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Fatou Bensouda kuacha kufanya uchunguzi katika mamlaka ya Palestina.

Bensouda alianzisha uchunguzi wa awali kuhusiana na hali ya Palestina mwaka 2015 na mnamo Machi 2021 mwendesha mashtaka mkuu huyo wa zamani akaanzisha uchunguzi rasmi. 

Wiki chache zilizopita, uchunguzi huu ulimpelekea mwendesha mashtaka wa sasa Karim Khan kuwasilisha ombi la waranti za kukamatwa kwa viongozi wa Israel na kundi la wanamgambo la Hamas.

Soma pia:Israel, Hamas zapinga waranti wa kukamatwa viongozi wao

Mnamo Mei 20, Khan alitangaza kwamba amewasilisha ombi la waranti wa kukamatwa kwa Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant na viongozi watatu wa kundi la Hamas.

Khan anazilaumu pande zote kwa kufanya uhalifu wa kivita katika mapigano yanayoendelea kwa sasa huko Gaza.

Uamuzi huo wa Khan umekosolewa pakubwa na Israel, Marekani na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Ripoti: vitisho kwa wafanyakazi wa ICC

Gazeti la The Guardian linaripoti kwamba vitisho vya mkuu wa zamani wa ujasusi wa Israel dhidi ya Bensouda, vilikuwa vinamlenga yeye mwenyewe pamoja na familia yake. 

Mwendesha Mshtaka Mkuu wa zamani ICC Fatou BensoudaPicha: Getty Images/AFP/ANP/B. Czerwinski

Gazeti hilo lakini linasema kwamba afisi ya Waziri Mkuu wa Israel iliyakanusha madai hayo na kusema kwamba ni ya ouongo.

Wachambuzi wanasema madai haya ni mazito na iwapo yatathibitika kuwa ya kweli basi mahakama ya ICC haiwezi kuyapuuza.

Ilipotakiwa kutoa tamko na DW, afisi ya mwendesha mashtaka wa ICC ilisema kwamba afisi hiyo pamoja na mahakama kwa ujumla zinakabiliwa na majaribio makubwa ya vitisho. 

Soma pia:Mwendesha mashtaka ICC aomba waranti dhidi ya Netanyahu, viongozi wa Hamas

Mnamo Machi 2022 afisi hiyo ilianzisha uchunguzi kuhusiana na mamadai ya uhalifu wa kivita unaofanyika Ukraine tangu mwaka 2013.

Mnamo Machi 2023, mahakama hiyo ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusiana na madai ya kutekwa nyara kwa watoto. Mahakama hiyo pia imetoa waranti wa kukamatwa kwa raia watatu wengine wa Urusi.

Uholanzi: Mahakama ipewe uhuru

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi kupitia taarifa amesema ni muhimu sana kwamba mahakama hiyo kupewa fursa ya kufanya kazi yake kwa njia huru na salama.

Mwanzoni mwa mwezi Mei kulipoanza tetesi kwamba kutatolewa waranti wa kukamatwa kwa viongozi wa Israel, afisi ya mwendesha mashtaka ilitoa taarifa ikionya dhidi ya majaribio ya kuizuia mahakama hiyo kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Soma pia:ICC yaonya dhidi vitisho vya ulipizaji kisasi kwa watendaji wake

ICC yaitunishia kifua Marekani

01:10

This browser does not support the video element.

Huko mjini Washington, maseneta wa chama cha Republican wametishia kuwawekea vikwazo maafisa wa mahakama ya ICC kutokana na hatua hiyo ya kutolewa kwa waranti wa kukamatwa kwa viongozi wa Israel. 

Ikumbukwe kwamba utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ulimuwekea vikwazo mwendesha mashtaka mkuu wa zamani Fatou Bensouda kwa kuanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya uhalifu wa kivita uliofanwa na Marekani nchini Afghanistan mnamo Septemba 2020.

Vikwazo hivyo lakini viliondolewa miezi michache baada ya Joe Biden kuchukua uongozi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW