1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaanza kuchunguza uhalifu katika maeneo ya Wapalestina

Daniel Gakuba
4 Machi 2021

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu -ICC imeanzisha uchunguzi rasmi katika uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanyika katika maeneo ya Wapalestina. Wapalestina wameikaribisha hatua hiyo, ambayo imepingwa vikali na Israel.

Fatou Bensouda Chefanklägerin am ICC
Mwendeshamashtaka Mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: ICC

Akianzisha rasmi uchunguzi huo, Mwendeshamashtaka mkuu wa mahakama ya ICC yenye makao yake mjini The Hague, Fatou Bensouda, amesema kesi hiyo itajikita katika mzozo wa mwaka 2014 kwenye Ukanda wa Gaza, ambao ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 2000. Bensouda amesema amefikia suluhisho kuwa zipo sababu za kutosha kuzishitaki pande zote zilizohusika, na kuongeza kuwa kipaumbele kwa mahakama ya ICC ni haki kwa wahanga, wawe Wapalestina au Waisraeli.

Soma zaidi:  ICC yafunguliwa njia kuchunguza uhalifu wa kivita maeneo yanayokaliwa na Israel

Mwendeshamashtaka huyo amesema uamuzi huu umefikiwa baada ya uchunguzi mgumu uliochukuwa miaka mitano, na kuapa kuwa uchunguzi utafanyika kwa uhuru, na bila hofu wala upendeleo.

Wapalestina wafurahia uamuzi wa ICC

Hazem Qassem, msemaji wa chama cha Hamas kinachoudhibiti Ukanda wa Gaza na ambacho kilipigana vita na Israel mwaka 2014, amesema wanakaribisha alichokiita uchunguzi juu ya uhalifu uliofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, na kuitaka mahakama ya ICC kusimama kidete mbele ya vitisho.

Watu zaidi ya 2000 waliuawa katika vita vya mwaka 2014 kati ya Israel na HamasPicha: picture-alliance/dpa

''Tunaitolea mwito mahakama ya ICC, ambayo tayari imeonyesha ujasiri kwa kuchukua uamuzi huu, kustahimili shinikizo inaloweza kuwekewa ili isitekeleze majukumu yake,'' amesema Qassem na kuongeza kuwa  badala yake, ICC inapaswa kusonga mbele katika ''kuwapa haki watu wetu na kuadhibu ukaliaji wa kimabavu wa Israel ambayo imeufanya uhalifu huu.''

Netanyahu adai uamuzi wa ICC ni chuki dhidi ya Wayahudi

Uamuzi huu wa ICC ni pigo kwa serikali ya Israel ambayo imekuwa ikifanya kampeni kabambe ya diplomasia ya mlango wa nyuma, kuzuia hatua hii ya kuanzisha rasmi uchunguzi juu ya uhalifu ambao yumkini umefanywa na wanajeshi wake. Mara moja baada ya ICC kutangaza bayana uamuzi wake, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliongoza mashambulizi dhidi ya mahakama hiyo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Yonatan Sindel/REUTERS

 ''Taifa la Israel limeshambuliwa jioni hii na ICC yenye upendeleo ambayo imefanya uamuzi wa kinafiki na wenye chuki dhidi ya Wayahudi. Ni uamuzi ambao unasema wapiganaji wetu mashujaa, wanaopambana na magaidi wabaya kabisa duniani, eti ni wahalifu, na kwamba kujenga makaazi katika mji mkuu wetu wa jadi wa Jerusalem, eti ni uhalifu wa kivita,'' amesema Netanyahu na kuongeza kwamba mahakama iliyoanzishwa kuzuia kutokea tena kwa uhalifu kama wa Wanazi dhidi ya Wayahudi, hivi sasa imeamua kuwalenga Wayahudi.

Soma zaidi:  Palestina yaifikisha Israel ICC

Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel imesema haikupendezwa na hatua hiyo ya ICC. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje mjini Washington Ned Price amesema Marekani itaendelea kusimama na Israel, na kupinga maamuzi yote yanayonuia kuilenga kwa njia zisizo halali.

 

afpe,ape