1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yafuta kesi dhidi ya Kenyatta

5 Desemba 2014

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC, Fatou Bensouda, ameifuta kesi dhidi ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kutokana kukosa ushahidi wa kutosha kuweza kumfungulia mashtaka.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya, Uhuru KenyattaPicha: Reuters/T. Mukoya

Hatua hiyo imefikiwa siku mbili baada ya majaji wa Mahakama ya ICC kuwapa waendesha mashtaka wiki moja kutoa ushahidi wa kutosha au kuifuta kesi ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu inayomkabili Kenyatta, na walisema kuwa kesi hiyo haiwezi kuendelea tena kuahirishwa.

Katika waraka ulioandaliwa kutoka kwenye makao makuu ya ICC iliyoko The Hague, Uholanzi, amesema kuwa upande wa mashtaka unafuta mashtaka dhidi ya Rais Kenyatta baada ya ushahidi kushindwa kuthibitisha wazi kuwa Rais Kenyatta alihusika na madai katika kiwango ambacho kinaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Wachambuzi wa masuala ya sheria wanasema kuwa tangazo hilo la ICC baada ya uchunguzi wa miaka minne uliogubikwa na kutishwa kwa mashahidi, rushwa na kutolewa ushahidi wa uwongo, litakuwa pigo kubwa kwa ofisi ya Bensouda na Mahakama ya ICC, iliyoanzishwa mwaka 2002 kuchunguza matukio ya uhalifu mkubwa duniani.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: AFP/Getty Images

Rais Kenyatta, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa anakabiliwa na mashtaka matano, ikiwemo mauaji, unakaji na kuwafukuza watu kwenye makaazi yao kwa madai ya kupanga ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mnamo mwaka 2007 hadi 2008, ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000 kukosa makaazi.

Rais Kenyatta afurahishwa na uamuzi wa ICC

Kwa upande wake Rais Kenyatta, ameelezea kufurahishwa kwake na tangazo hilo la ICC la kumfutia kesi dhidi yake na kwamba amekuwa akizisubiri habari hizo kwa muda mrefu. Katika ujumbe aliouandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Kenyatta amesema anataka pia mashtaka dhidi ya makamu wake William Ruto yafutiliwe mbali.

''Nataka kurudi nyumbani haraka kwa mke wangu niweze kumwambia habari hizi nzuri'', alisema Kenyatta. Rais Kenyatta alizungumuzia tangazo hilo la ICC wakati akiwa kwenye mkutano wa maafisa na wafanyabiashara wakubwa. Amesema kesi moja imeshafutwa, sasa bado kesi mbili.

Makamu wa Rais wa Kenya, William RutoPicha: picture alliance / Kyodo

Awali, waendesha mashtaka walilalamika kuwa Rais Kenyatta alikuwa hatoi ushirikiano wa uchunguzi wa kesi inayomkabili. Katika baruapepe aliyoiandika kwa shirika la habari la AFP, wakili wa Kenyatta, Steven Kay, amesema Mahakama ya ICC, inapaswa kumuomba radhi kiongozi huyo wa Kenya kutokana na kufungua kesi iliyozingatia ushahidi wa uwongo.

Aidha, wakili wa wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi, Fergal Gaynor, ameishutumu serikali ya Kenyatta kwa kuizuia mahakama ya ICC na kwa kuwavunja moyo maelfu ya watu ambao wameathirika na ghasia hizo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, APE,DPAE,RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW