ICC yafuta kesi ya Kenyatta
5 Desemba 2014Fatu Bensouda amesema katika waraka uliyoandaliwa kutoka makao makuu ya mahakama hiyo ilioko The Hague kwamba upande wa mashtaka unafuta mashtaka dhidi ya Kenyatta kutokana na ushahidi kushindwa kuthibitisha bila ya kasoro madai ya kuhusika kwa Kenyatta katika kiwango kilichofikia kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Tangazo hilo la kufadhaisha siku mbili baada ya majaji wa mahakama ya ICC kuwapa waendesha mashtaka wiki moja kuyapa nguvu madai yao ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu au kuyaondoa kwa kusema kwamba kesi hiyo haiwezi kuendelea tena kuahirishwa. Kenyatta mwenye umri wa miaka 53 alikuwa akikabiliwa na mashtaka matano yakiwemo mauaji,ubakaji na kuwaondoa watu kwenye makazi yao kwa madai ya kupanga ghasia za baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki hapo mwaka 2007- 2008 ambapo zaidi ya watu 1,200 wameuwawa na wengine 600,000 kupotezewa makazi yao. Wataalamu wa kisheria wanasema tangazo hilo baada ya uchunguzi wa miaka minne uliogubikwa na kutishwa kwa mashahidi,rushwa na kutolewa kwa ushahidi wa uwongo litakuwa pigo kubwa kwa ofisi ya Bensouda na mahakama ya ICC yenye makao yake The Hague ilioanzishwa mwaka 2002 kuchunguza matukio ya uhalifu mkubwa duniani.
Mwandishi: Mohamed Dahman
Mhariri: Saumu Yusuf