ICC yasikiliza hoja katika kesi dhidi ya Ongwen
21 Januari 2016Waendesha mashataka wa ICC wanamtuhumu Ongwen kuwa kamanda wa ngazi ya juu katika kundi la Lords Resistance Army linaloongozwa na Joseph Kony ambalo linadaiwa kuhusika na mauaji ya kinyama katika kambi za wakimbizi nchini Uganda mwaka 2003 na mwaka 2004.
Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita ICC iliyoko nchini Uholanzi itasikiliza hoja za pande zote katika kesi ya uhalifu wa kivita inayomkabili aliyekuwa kamanda mkuu wa kundi la LRA nchini Uganda Dominic Ongwen.Anakabiliwa na mashtaka 70 ikiwemo mauaji,ubakaji,utesaji na kuwalazimisha wanawake kuolewa pamoja na kuwatumikisha jeshini watoto waliotekwa kwenye makambi ya wakimbizi yaliyoshambuliwa na kundi hilo mwaka 2003 na 2004 na yeye akihusika.
Ongwen hatohitajika kujibu chochote kuhusu tuhuma zinazomkabili hadi palesi kesi itakapoanza rasmi ikiwa mahakama itapitisha uamuzi wa kutoa tarehe ya kuanza kwa kesi hiyo baada ya kuutathmini ushahidi wa hoja zitakazotolewa leo.Maria Mabinti Kamara ni mratibu wa shughuli za mahakama hiyo ya ICC anayehusika na kesi za Afrika amefafanua zaidi kuhusu kitakachofanyika hii leo
''Upande wa mashataka wa ICC utafungua kikao hicho kwa kutoa hoja zao za ushahidi,Mawakili wa waathiriwa walioruhusiwa watakuwa na muda pia wakutoa hoja zao na kufuatiwa na wakili wa upande wa utetezi ambaye ni Ayina Odongo kuhakikisha kwamba haki za bwana Ongwen zinaheshimiwa katika mchakato wote na mwishoni mwa mchakato mzima majaji watakwenda mapumzikoni na kutoa uamuzi baada ya siku sitini''
Kimsingi vikao vya kuskiliza hoja vinavyoanza leo vitachukua muda wa siku tano ambapo vinatarajiwa kumalizika tarehe 27. Mchakato huu unaoanza leo ni muhimu sana na pia ni mtihani kwa waendesha mashataka ambao wanalazimika kuwashawishi majaji kwamba kesi yao ya muongo mmoja ambayo wamekuwa wakiifanyia uchunguzi na kukusanya ushahidi tangu Ongwen alipojisalimisha mwaka mmoja uliopita,ina mashiko na nguvu ya kutosha kupewa nafasi ya kusikilizwa kikamilifu kwa kuzingatia ushahidi uliopo.Kwa mujibu wa Maria Mabinti mratibu wa ICC kuna mambo matatu yanayotarajiwa mwishoni mwa mchakato huu kuhusu kesi hiyo.
''Kwa kuzingatiwa tathmini ya ushahidi utakaowasilishwa majaji wanaweza kuthibitisha kwamba kuna kesi ya kujibu mashtaka ama yote au baadhi.Wanaweza pia kuamua kwamba hakuna kesi ya kujibu au kuakhirishwa kwa kesi hiyo na kuwataka waendesha mashataka wa mahakama hiyo kufanya uchunguzi zaidi.''
Mawakili wa Ongwen wanatarajiwa kutia msukumo katika kikao kitakachoendelea wiki ijayo kutaka mashataka yanayomkabili Ongwen yafutiliwe mbali.Mashirika ya haki za binadamu yanaema kwamba kundi la LRA limekuwa likihusika na mauaji ya kinyama dhidi ya raia katika eneo kubwa la Afrika mashariki na Afrika ya Kati.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef