ICC yataka mdahalo kuzuia Afrika kujitoa
25 Oktoba 2016Siku chache baada ya Afrika Kusini na Burundi kutangaza kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ya mjini The Hague, Uholanzi, sasa Mahakama hiyo inataka mdahalo na mataifa hayo na mengine yenye azma kama hiyo ikisema imesikitishwa na hatua hiyo huku zikiweko khofu hasa kwa upande wa mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani kwamba nchi za Kiafrika huenda zikaanza kujiondowa kwa wingi kutoka ICC.
"Ni masikitiko makubwa katika bara la Afrika" hivyo ndivyo alivyosema Rais wa Baraza la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo ya ICC hapo jana, kufuatia uamuzi wa Burundi na Afrika Kusini kujiondoa kwenye chombo hicho cha kimataifa cha sehria dhidi ya wahalifu wa kivita.
Sidiki Kaba, ambaye pia ni waziri wa sheria wa Senegal, amesema jumuiya ya kimataifa itafanya kila iwezalo kuchukua hatua kabambe za kuhakikisha kwamba nchi hizo mbili zinatafakari upya hatua ilizochukua, akisisitiza kutumia njia ya majadiliano kulitatua hilo.
Jijini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema naye amesikitishwa na uamuzi wa Afrika Kusini kujiondoa ICC na kuitolea mwito nchi hiyo kufikiria tena uamuzi wake huo kabla ya kuanza utekelezaji wa kujiondoa kwake katika chombo hicho.
Akitoa msimamo huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, msemaji wake, Stephane Dujarric, amesema Ban Ki-moon anaaamini kwamba ICC ni chombo kikuu duniani kinachofanya juhudi za kupambana na viongozi au watu wasioshtakiwa kutokana na nafasi zao. "Kadhalika ni chombo kinachofanya juhudi kubwa kukabiliana na mizozo," amesema Dujarric.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Richard Dicker, pia ameitolea wito Afrika Kusini kuangalia upya msimamo wake. Afrika Kusini ilitangaza siku ya Ijumaa kwamba itajiondoa ICC, ikisema uanachama wake ndani ya chombo hicho unazuia juhudi za kusaidia kuitatua migogoro katika bara la Afrika.
Burundi nchi inayozongwa na mgogoro, ilipiga kura kupitia bunge kuunga mkono kujiondoa ICC na wiki iliyopita Rais Pierre Nkurunziza akaweka saini kwenye azimio hilo.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisheria na siasa katika bara la Afrika wanahisi kwamba bara hilo linataka kuonesha ubabe wake mbele ya jumuiya ya kimataifa kwa kuzipinga taasisi za jumuiya hiyo ili kuendeleza ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na kutowajibikia uhalifu wanaoufanya dhidi ya wananchi wao.
Hata hivyo mitazamo pia inatofautiana kuhusu dhima ya mahakama ya ICC kuelelekea bara la Afrika na viongozi wake. Barani Afrika hisia zilizoenea ni kwamba mahakama hiyo imekuwa ikiwaandama kionevu viongozi wa kiafrika kuliko inavyofuatilia masuala ya mabara mengine.
Mwandishi: Saumu Yussuf/AP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef