1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC imetoa waranti wa kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin

18 Machi 2023

Mahakama ya Kimataifa yenye kuhusika na Jinai (ICC) imetoa waranti wa kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa uhalifu wa kivita, ikimtuhumu kwa uwajibikaji wa kibinafsi kwa utekaji nyara wa watoto nchini Ukraine.

Russland | Kongress der Union der Industriellen und Unternehmer | Wladimir Putin
Picha: Ramil Sitdikov/SNA/IMAGO

Mahakama ya Kimataifa yenye kuhusika na Jinai (ICC) imetoa waranti wa kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa uhalifu wa kivita, ikimtuhumu kwa uwajibikaji wa kibinafsi kwa utekaji nyara wa watoto nchini Ukraine.

Hatua hiyo ni ya kwanza kutokea kwa mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa dhidi ya mmoja wa viongozi mataifa wanachama watano wa kudumu wa baraza Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake ICC imesema Putin anadaiwa kuwajibika na uhalifu wa kivita kwa kufanya uhamisho haramu wa watoto kutoka maeneo waliyoyanyakua kwa Ukraine. Mahakama hiyo pia imetoa hati ya kukamatwa kwa Maria Lvova-Belova, kamishna wa Haki za Watoto katika Ofisi ya Rais wa Urusi.

Mwezi Oktoba Shirika la habari la AP liliandika ripoti kuhusu kuhusika kwake katika kuwateka watoto yatima wa Kiyukrein, ukiwa uchunguzi wa mwanzo, ambao ulifuatiliwa hadi ndani ya Urusi kwa kukusanaya ushahidi kadha wa kadha.

Urusi yaipuuza hatua hiyo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sergei VershininPicha: Russian Foreign Ministry/dpa/picture alliance

Hatua hiyo mara moja imepuuziliwa mbali na Urusi huku kwa uopande mwingine ikipokelewa kwa heri na Ukraine. Matokeo yake yanaonekana kama kuwa madogo, na hasa kwa Rais Putin kupanda kizimbani mjini The Hague kwa kuwa serikali ya Moscow haitambui kisheria mamlaka ya mahakama hiyo.

Lakini laana ya kimaadali inaweza kumweka katika wakati mgumu kiongozi huyo wa Urusi katika maisha yake yote na pia kumweka katika kipindi kigumu katika siku za usoni pale anapokwenda kuhudhuria mikutano ya kilele katika mataifa ambayo sheria inayataka yamtie nguvuni.

Adil Ahmad ambae ni mjuzi katika sheria za kimataifa anasema "Putin anaweza kwenda China, Syria, Iran na kwa washirika wake wachache, lakini hawezi kwenda katika maeneo mengine na hatokwenda katika mataifa wanachama ambayo anaamini yatamkamata". Alisema mtaalamu huyo.

David Crane, mwendesha mashtaka wa kimataifa wa zamani, aliliambia shrika la habari la AP kwamba Vladimir Putin anatazamwa kama mtu aliyepoteza uaminifu wake kisiasa duniani. Na kiongozi yeyote anaeshirikiana nae atawajibishwa pia.

ICC yasema Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kumkamata Putin

Kupitia taarifa yake kwa njia ya video Rais wa Mahakama ya ICC, Piotr Hofmanski amesema majaji wa mahakama hiyo wametoa waranti lakini litakuwa jukumu la jumuiya ya kimataifa kuitekeleza. Mahakama hiyo haina polisi wake ambao wanaweza kulisimamia zoezi hilo.

Soma zaidi: Rais Vladmir Putin amempokea rais wa Syria Bashar al-Assad

Kwa mujibu wa mkataba ambao umeiunda mahakama hiyo,"Mkataba wa Roma" kwa zingatio la kuwatia katika mkono wa kisheria viongozi wa kisasa na wahusika wengine wa mikasa mikubwa ya ukatili, uhalifu wa kivita na mauawji ya wengi, mtuhumiwa akikutwa na hatia anaweza kutumikia hata kifungo cha maisha gerezani.

Chanzo AP