1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatoa agizo la kukamatwa kamanda mmoja wa Libya

16 Agosti 2017

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, imetoa agizo la kukamatwa Kamanda Mahmoud al Warfalli wa kikosi cha kupambana na wapigananji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) nchini Libya kwa tuhuma za mauaji.

Fatou Bensouda Chefanklägerin am ICC
Picha: ICC

Kamanda Mahmoud al Warfalli anakiongoza kikosi kinachopigana upande wa Jemadari Khalifa Hiftar mashariki mwa Libya, kikosi ambacho kinaungwa mkono pia na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, amesema vitendo vya mateso, dhuluma na hatimaye kuuwawa kinyama kwa watu waliokuwa hawana hatia vinapaswa kupigwa vita na kutokomezwa. Bensouda ameutaka utawala wa Libya kumfikisha al Warfalli mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa.

Mji wa BenghaziPicha: Reuters/E.O. Al-Fetori

Kamanda Al- Warfalli, ambaye yeye mwenyewe ni Muislamu mwenye itikadi kali, anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya watu kadhaa katika mji wa Benghazi ulio mashariki mwa Libya. Miili mingine ya watu hao waliouwawa ilikutwa kwenye majalala katika mji huo ikiwa imekatwa viungo, huku ikiwa na alama za kupigwa risasi vichwani.

Taarifa kutoka kwenye mahakama hiyo ya kimataifa zinasema kuwa al Warfalli ameonekana mara nyingi katika vidio zinazotumwa kwenye mitandao kwa mfano kwenye vidio ya tarehe 3 mwezi wa Juni, akiwa anamwamrisha mtu aliyekuwa amevalia vazi lililokuwa limemfunika uso ainue mikono yake juu kabla ya kumpiga risasi. Hata baada ya mtu huyo kuanguka chini al Warfalli alionekana akiusogelea mwili wa mtu huyo na kuendelea kuupiga risasi mara kadhaa huku akisema "Uliongozwa na shetani."

Tuhuma zinazo mkabili kamanda al- Warfalli

Baadhi ya watu anaotuhumiwa kuwauwa inasemekana walikuwa ni wafuasi wa makundi ya Al Qaida na Ansaar al Shariah, kundi linalolaumiwa kuhusika na mashambulizi ya mwaka 2012 dhidi ya ubalozi wa Marekani katika mji wa Benghazi ambako balozi wake, Chris Stevens, aliuwawa. Mapema mwaka huu, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilimtaka Jemadari Khalifa Hiftar achunguze malalamiko kwamba kikosi chake kilitenda mauaji na dhuluma za kivita. Libya ni taifa lililotumbukia kwenye mzozo mnamo mwaka 2011 baada ya kuanzishwa maandamano ya kumpinga na hatimaye kumng'oa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muammar Gadaffi, aliyeuwawa baadaye. Hadi leo, taifa hilo tajiri kwa mafuta limegawanyika na kuwa na mabunge na serikali mbili - moja ya upande wa mashariki na nyingine ya magharibi, zote zikiungwa mkono na makundi ya wapiganaji tofauti wa makabila pamoja na makundi ya kisiasa.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef   

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW