1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICJ yaiunga mkono Somalia katika mzozo na Kenya

Shisia Wasilwa12 Oktoba 2021

Mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJ iliyoko, imeiunga mkono Somalia katika mzozo wa mpaka wa bahari ya Hindi kati yake na  Kenya, katika kesi ambayo inaathiri eneo linalodhaniwa kuwa na hifadhi kubwa ya maufa na gesi.

Militärmanöver Malabar 2018 Indien Australien USA Japan
Picha: U.S. Navy/abaca/picture alliance

Uamuzi huo wa Jumanne unafungamanisha kisheria, inagwa mahakala hiyo ya Umoja wa Mataifa haina mamlaka ya utekelezaji. 

Jopo la majaji 15 likiongozwa na jaji wa Marekani Joan Donoghue lilitoa uamuzi huo katika Peace Palace iliyoko Hague. 

Kenya ilikuwa inataka, mpaka huo usalie jinsi ulivyo huku Somalia ikitaka ufanyiwe marekebisho.

Mahakama hiyo imesema kuwa Kenya ilikiuka makubaliano yote ambayo yalifikiwa na Somalia, mwaka 1979. Kenya kwa upande wake imekuwa ikisema kuwa eneo linalozozaniwa limekuwa himaya yake tangu mwaka huo.

Eneo hilo la bahari linalozozaniwa, lina ukubwa wa kilomita za mraba 100,000 sawa na takriban maili 40,000 za mraba.

Mikutano miwili ilifanyika mwaka 2014 kutafuta mwarubaini, lakini hakuna hatua iliyopigwa. Awamu nyingine ya mkutano iliyofuatia mwaka huo ilishindwa baada ya ujumbe wa Kenya kukosa kuhudhuria, bila kuufahamisha upande wa Somalia.

Eneo la bahari linalozozaniwa ninadaiwa kuwa na utajiri wa gesi na mafuta.Picha: Isabela Le Bras/AP/picture alliance

Somalia iliwasilisha kesi hiyo mahakamani mwaka 2014, baada ya kudai kuwa juhudi za kidiplomasia kutatua mzozo huo ziligonga mwamba.

Somalia haijawa na serikali imara tangu mwaka 1991 wakati utawala wa rais Siad Barre ulipopinduliwa, majaji wakisema kuwa suala hilo lilizingatiwa wakati wa kutoa uwamuzi huo.

Tayari Nairobi imeipa kampuni ya nishati ya Italia zabuni ya kuchimba mafuta na gesi katika eneo linalozozaniwa, hatua ambayo Somalia inapinga.

Mahakama hyo imesema kuwa mipaka kati ya kenya na Somalia inastahili kuzingatia mwafaka wa 1927 na 1933.

Mahakama hiyo imezikosoa Somalia na Kenya kwa kutoafikiana kuhusu mpaka unaozozaniwa.

Majuma mawili yaliyopita, Kenya ilifamhamisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress juu ya nia yake ya kujiondoa kutoka azimio la mwaka 1965 chini ya Mahakama ya Haki ya Kimataifa. 

Mabunge ya Taifa na Seneti nchini Kenya, tayari yameshamuomba Rais Kenyatta kuwatuma wanajeshi iwapo sehemu yoyote ya Kenya ikiwemo eneo linalozozaniwa na Somalia litakabiliwa na kitisho, tamko ambalo limekosolewa na Mahakama ya Kimataifa ya ICJ. Peter Kagwanja ni mtaalamu wa masuala ya kidiplomasia.

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya haki (Picha ya maktaba)Picha: picture-alliance/AP

"Mahakama ya ICJ ni mahakama ya kusuluhisha, sio mahakama ambapo haki hutekelezwa. Huwezi kusuluhisha mzozo wa majirani wawili ambao hawajazungumza. Unasuluhisha nini? Somalia haijawahi kupinga eneo hilo kuwa la Kenya, ili kuingilia himaya ya Kenya kwa kipindi kirefu,” amesema Kagwanja

Mwaka 2009, Kenya na Somalia zilisaini mwafaka, ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu mipaka. Mwaka 2014, Somalia iliamua kusuluhisha mzozo huo katika mahakama ya ICJ, iliyoko The Hague. Kenya inashikilia kuwa mahakama ya ICJ haina mamlaka na uwezo wa kufanya uamuzi wa eneo linalozozaniwa.

Mataifa ya Kenya na Somalia yatalazimika kurejea kwenye meza ya mazungumzo kutatua mzozo huo ambao umedumu kwa kipindi cha miaka saba sasa.