1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICRC: Vituo vya afya vimeelemewa mno huko Gaza

18 Julai 2024

Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya siku ya Alhamisi kuwa vituo vyote vya afya kusini mwa Gaza viko katika hali mbaya kutokana na ongezeko la mashambulizi ya Israel na idadi kubwa ya majeruhi.

Wanawake wa Kipalestina wakiwa na mtoto mgonjwa katika hospitali ya Nasser, Gaza
Wanawake wa Kipalestina wakiwa na mtoto mgonjwa katika hospitali ya Nasser, GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema kuwa hospitali yake ndogo katika mji wa Rafah imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa hospitalini kutokana na majeraha yanayosababishwa na mashambulizi.

Shirika hilo la kimataifa limesema kuwa hospitali nyingi katika eneo hilo zimeelemewa, jambo ambalo litapelekea hivi karibuni madaktari kulazimika kufanya "maamuzi magumu" ya kuchagua ni nani anayepaswa au la kutibiwa.

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani

Wiki iliyopita, watu 850 wanaohitaji huduma waliwasili katika hospitali hiyo inayomilikiwa na shirika la Msalaba Mwekundu, huku karibu nusu ya watu hao wakiwa ni wanawake na theluthi moja wakiwa ni watoto.

Wapalestina wakiubeba mwili wa jamaa yao aliyeuawa huko Khan Younis, GazaPicha: Jehad Alshrafi/AP/picture alliance

Taarifa ya shirika hilo imebainisha kuwa wagonjwa wengi wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na wamekuwa wakiishi katika mazingira duni yenye msongamano wa watu na yanayokabiliwa na uhaba wa chakula na maji safi, jambo linalowaweka hatarini zaidi kupata magonjwa.

Kiongozi wa Israel ashinikiza kuendeleza mashambulizi

Waziri wa Usalama wa Israel na mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben Gvir, ameutembelea leo  msikiti wa Al Aqsa  huko Jerusalem ambao umekuwa kiini cha mvutano kati ya Israel na Palestina na kusema:

"Nimekuja hapa, mahali muhimu kwa taifa la Israel, kwa watu wa Israel, mnatakiwa kuwaombea mateka warudi nyumbani lakini si kwa makubaliano ya kizembe, bila kujisalimisha. Ninaomba na pia kufanya kazi kwa bidii ili Waziri Mkuu Netanyahu awe na ujasiri wa kutoachia msimamo wake na kuelekea kwenye ushindi  kwa kuongeza shinikizo la kijeshi, na kuzima ari ya Hamas kushinda."

Waziri wa Usalama wa Israel na mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben GvirPicha: Debbie Hill/UPI Photo/IMAGO

Kauli ya Ben Gvir imetafsiriwa kuwa huenda inatishia kuvuruga mchakato unaoendelea wa mazungumzo ya usitishwaji mapigano, hasa wakati huu mashambulizi ya Israel yakiendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali huko Gaza.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema hivi leo kwamba  umwagaji damu huko Gaza  ni lazima usitishwe sasa, akiongeza kuwa raia wengi mno katika eneo la Palestina wamepoteza maisha yao kutokana na jibu la Israel kwa ugaidi wa kikatili wa Hamas. Von der Leyen alikamilisha kwa kusema, watu wa Gaza hawawezi kuvumilia zaidi na ubinadamu hauwezi tena kustahimili.

(Vyanzo: Mashirika)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW