1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran wanarejea nyumbani

ELIZABETH KEMUNTO2 Septemba 2004

Wakimbizi wapatao milioni moja wamerejea nchini Afghanista kutoka nchi jirani Iran ambako walitorokea wakati nchi yao ilipovamiwa na Marekani.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi (UNHCR), Ruud Lubbers, amesema wakimbizi hao wanahitajika katika kujenga upya nchi yao.
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi (UNHCR), Ruud Lubbers, amesema wakimbizi hao wanahitajika katika kujenga upya nchi yao.Picha: AP

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, limetangaza kuwa kufikia sasa wakimbizi milioni moja wamerejea nyumbani kwao Afghanistan kutoka Iran. Shirika hilo lilianza mpango wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi kwa hiari yao mnamo Aprili 2002. Idadi hiyo inaonekana kupanda zaidi kwa sababu ya uchaguzi ambao unakarabia kufanywa mwezi Oktoba nchini humo.

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi, Ruud Lubbers, amesema ana wasiwasi kuhusu hali ya usalama wa ndani wa nchi hiyo, lakini wakati huo huo, amekaribisha idadi hiyo ya wakimbizi wanaorejea nyumbani na kusema kuwa ni hatua kubwa kwa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Iran pia inafurahia idadi ya wakimbizi hao ambao wanarudi nchini Afghanistan, kwani bado ina wakimbizi wa asili ya Afghanistan wapatao milioni moja, ambao wanatarajiwa kurudi makwao. Ingawa Waafghanistan hao walisaidia kufanya kazi ndogo ndogo nchini Iran, Wairan wana hamu kubwa ya kuwaona wameondoka na kurudi Afghanistan.Bwana Lubbers alisema utaratibu wa kujenga upya nchi baada ya vita ni mrefu na mgumu lakini aliongeza kuwa idadi hiyo ya watu milioni moja waliorejea watahusika katika ujenzi upya wa Afghanistan mbali na kujenga maisha yao binafsi.

Katika wiki chache zilizopita, kadri Waafghanistan elfu nne wamefunga safari ya kurudi nyumbani. UNHCR imesema kuwa wakimbizi wengi wamevutiwa na nafasi za kazi na mishahara ya juu, watakaporudi nchini kwao.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Iran Phillipe Lavanchy, amesema kuwa wakimbizi wengi wa kutoka Afghanistan ambao wako nchini Iran, wamesoma na wana ujuzi unaotakikana kwa nchi yao kwa siku za usoni. Bwana Lavanchy aliongeza kuwa kila mwalimu atakayerejea atawafunza watoto kusoma, na kila daktari atayaokoa maisha ya watu na hawa watakuwa sehemu muhimu ya kujenga upya Afghanistan.

UNHCR imewasaidia wale wakimbizi ambao wako tayari kurudi makwao kwa kuwapa usafirishaji wa bure pamoja na pesa taslimu za kununua chakula baada ya kufika nyumbani. Wakimbizi hao pia wanaandikishwa katika miradi ya kutoa misaada baada ya kurejea nchini kwao.

UNHCR vile vile imeanzisha kamati za kutatua mizozo katika miji saba nchini Iran. Kamati hizi zinanuiwa kuwasaidia wakimbizi kutatua mizozo ya kisheria kabla ya kuondoka nchini humo.Mizozo hii ni kama vile kukosa kulipwa mishahara au kukataa kwa baadhi ya wenye nyumba kurudisha fedha walizozitoa kama rubuni kabla ya kuingia katika nyumba hizo.

Shirika hilo la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa hata hivyo linakabiliwa na jukumu lingine la kuwalinda wakimbizi ambao hawataki kuondoka nchini Iran. Shughuli za kuwaregesha nyumbani wakimbizi sio za kuwalazimisha kufanya hivyo kwani kuna ripoti kuwa baadhi ya wakimbizi wamefukuzwa ingawa wana hati za kuwaruhusu kukaa nchini Iran. Duru kutoka mashirika mengine ya misaada zinasema kuwa wakimbizi katika maeneo fulani wamelazimishwa kurudi nchini Afghanistan lakini Iran imekanusha madai hayo.

Bwana Lavanchy amesema hatua zinachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.

Ikiwa mtindo wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao utaendelea, UNHCR inakadiri kuwa wakimbizi wengine laki mbili watakuwa wamerejea Afghanistan kufikia machi mwaka ujao, ambao ndio wakati mpango huu wa kuwarejesha wakimbizi makwao umepangwa kumalizika.

Idadi ya wakimbizi watakaokuwa nchini Iran baada ya wakati huo itakuwa kadri laki nane na shirika hili la wakimbizi linashirikiana pamoja na serikali ya Iran ili kupata suluhisho la muda mrefu kwa wakimbizi hao watakaobaki nchini Iran.

Njia moja ambayo tayari inajadiliwa ni ile ya kuanzisha mfumo wa uhamiaji baina ya Iran na Afghanistan, ambao utawaruhusu Waafghanistan kuwa na hati za kufanya kazi nchini Iran.

Wengi miongoni mwa wanaosita kurudi nyumbani, wanafanya hivyo kutokana na wasi wasi wa ukosefu wa usalama nchini mwao, Afghanistan.

Mapigano kati ya makundi yanayohasimiana, yalisababisha maelfu ya wakimbizi kukwama katika mpaka na Iran kwa muda wa siku tatu mnamo mwezi uliopita. Mapigano hayo yalitokea katika mji wa Herat, magharibi mwa nchi hiyo. Hofu ya usalama si suala linalowasumbua wakimbizi pekee bali hata mashirika ya misaada ya kimataifa. Itakumbukwa kwamba tarehe 4 Agosti, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, lilisitisha harakati zote kusini mashariki mwa Afghanistan, baada ya watumishi wawili wa shughuli za usamabazaji misaada wa shirika la kijerumani MALTESER kuuwawa kwa kupigwa risasi katika wilaya ya PAKTIA, lakini hivi sasa shughuli hizo zimeanza tena kama kawaida.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW